Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka amezindua mashindano ya taifa ya mpira wa kikapu na kusema kuwa Simiyu imedhamiria kuleta mapinduzi katika sekta ya michezo kama njia kukuza vipaji na kuongeza ajira kwa vijana.
Akizindua mashindano hayo yanayofanyika kwa mara ya kwanza katika uwanja wa halmashauri ya mji wa bariadi, Mhe Mtaka amesema mashindano hayo ni kielelezo cha jitihada za mkoa wa Simiyu katika kuhakikisha unatumia michezo kama biashara na kuondokana na utamaduni wa kutumia michezo kujiburudisha.
Mtaka ameongeza kuwa mashindano haya yatatumika kama darasa litakalo uwezesha mkoa kujipanga vizuri na kuandaa timu zake kwa mashindano yajayo huku akisisitiza kuwa mkoa wa Simiyu utaendelea kuibua fursa mbalimbali kupitia michezo kama njia kukuza uchumi na kuimarisha mahusiano ya kijamii.
“Bila shaka nyote mmejionea jinsi tulivyo wekeza kwa gharama kubwa, tumetengeneza uwanja huu wenye ubora wa kipekee nchini, naomba niwahakikishie tutautumia kikamilifu kuleta mapinduzi ya mchezo wa mpira wa kikapu mkoani kwetu hasa kwa kuibua vipaji vipya, pia tutatumia mashindano ya UMISHUMTA na UMISETA kupata timu bora ambayo ninaamini ndio watakuwa mabingwa wa baadae wa mchezo huu, alisisitiza Mtaka”.
Adha Mhe Mtaka amemwagiza afisa elimu wa mkoa kuandaa mpango wa kuboresha mchezo huo ikiwa ni pamoja na kuwabaini na kuwatumia walimu wenye uwezo wa kufundisha mpira wa kikapu ili waweze kuziandaa timu za mkoa kwa mashindano mbalimbali.
Kwa upande wake Makamu wa rais wa shirikisho la mpira wa kikapu nchini Mboka Mwambusi amesema kutokana na mchango mkubwa wa mkuu wa mkoa wa Simiyu katika kufanikisha mashindano hayo, shirikisho hilo limeamua kuyaita mashindano ya taifa ya mpira wa kikapu ya Mtaka.
“Sote ni mashuhuda wa jitihada za mheshimiwa Anthony Mtaka katika kufanikisha mashindano haya, mtakumbuka tulihangaika sana kutafuta mkoa utakaoratibu shughuli hii, ni Simiyu pekee ndio walikubali kwa moyo mkunjufu, hivyo tumeona zawadi pekee ni kuyapa jina la aliyefanikisha zoezi hili, aliongeza Mwambusi”.
Naye Katibu wa Shirikisho la mpira wa kikapu nchini Bakari Ramadhani amesema mashindano hayo yatatumika kama chachu ya kuibua vipaji vipya halikadhalika yatatumika kuwapata wachezaji bora watakaounda timu ya taifa ya mpira wa kikapu kwa siku za baaadae.
Mashindano hayo yanayoshirikisha timu kutoka mikoa 8 yanatarajiwa kuhitimishwa tarehe 22 Disemba ambapo mshindi atakabidhiwa kikombe.
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa