Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini amezindua rasmi utafiti unaohusu matumizi ya simu za mikononi katika kuongeza ulipaji kodi za majengo nchini Tanzania, PIERI 20355 ambao utafanyika kuanzia Novemba 28, 2019 hadi 30 Juni 2020 katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi na Halmashauri ya Wilaya ya Busega.
Akizindua utafiti huo Novemba 28, 2019 mjini Bariadi Sagini amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri hizo kutoa ushirikiano unaotakiwa kwa watafiti ili kuwawezesha kufanya kazi yao kwa ufanisi na kupata matokeo sahihi.
“ Wakurugenzi katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi na Busega, hakikisheni mnatoa ushirikiano katika utafiti kwani majengo yanayolipiwa kodi ya majengo yapo kwenye maeneo yenu na wamiliki wa majengo hayo pia wapo katika maeneo yenu,” alisema Sagini.
Sagini amewaahidi watafiti ushirikiano mkubwa ili utafiti ufanyike kama ilivyokusudiwa kwa lengo la kuongeza mapato yatokanayo na kodi ya majengo huku akiwaomba watafiti hao kuendeleza kushirikiano na mkoa wa Simiyu katika tafiti mbalimbali kwa maendeleo ya Mkoa, wananchi na Taifa kwa ujumla.
Akiwasilisha taarifa ya utambulisho wa utafiti huo Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Mzumbe na Mtafiti Mwandamizi wa Utafiti huu, Dkt.Francis Mwaijande, amesema Matokeo ya utafiti huu yatawezesha mamlaka za maamuzi ziweze kutoa maamuzi kwa kuzingatia taarifa zilizifanyiwa utafiti na hivyo kuwa na maamuzi ya kuongeza ufanisi kwenye ukusanyaji kodi.
Ameongeza kuwa matokeo ya utafiti huu yanatarajiwa kuongeza mapato yatokanayo na kodi za majengo kwa Serikali kwa kuhamasisha ulipaji kodi kwa kutumia simu zao za mkononi kwa njia ya meseji.
Utafiti unaohusu matumizi ya simu za mikononi katika kuongeza ulipaji kodi za majengo nchini Tanzania, PIERI 20355 unafanyika kwa lengo la kutafuta Ushahidi wa kitaaluma ili kuainisha kipi kinaweza kuongeza ulipaji kodi kwa kufuata sheria.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2019/11/ras-simiyu-azindua-utafiti-wa-matumizi.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa