Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini amewataka watumishi wa Umma mkoani humo kuwa mabalozi wema wa maadili ya utumishi wa umma katika maeneo ya kazi ikiwa ni pamoja na kutopokea zawadi kwa wananchi wanaowahudumia kwa kuwa wanalipwa mshahara na Serikali kwa kazi hizo.
Sagini ameyasema hayo Machi 14, 2019 Mjini Bariadi wakati akifungua mafunzo ya Kamati za Kudhibiti Uadilifu za Mkoa wa Simiyu, yanayoendeshwa na Mratibu wa Utawala Bora kutoka Ofisi ya Rais kwa kushirikiana na Maafisa kutoka TAKUKURU na Ofisi ya Rais TAMISEMI.
Amesema watumishi wa umma wanalipwa mishahara ili waweze kuwahudumia wananchi hivyo hawapaswi kudai chochote kutoka kwa wananchi.
"'Acheni kupokea vizawadi vidogo vidogo kwa huduma tunazotoa kwa wananchi ambazo tunalipwa mshahara kutokana na huduma hizo; muwe mabalozi wa kueneza maadili mema kwa watumishi wenzenu na nje ya maeneo yenu ya kazi ili ofisi zetu za Umma mkoani Simiyu ziwe mfano wa kuigwa" alisema Sagini.
Aidha, Sagini amezitaka kamati zote za kudhibiti uadilifu mkoani Simiyu mara baada ya mafunzo ziandae mpango kazi wa namna ya kushughulikia kero mbalimbali za watumishi zinazohusiana na ukiukwaji wa maadili katika utumishi wa Umma, ili kuwa na watumishi wanaozingatia sheria, kanuni na miongozo mbalimbali ya Utumishi wa Umma.
Akitoa taarifa ya mwenendo wa makosa ya rushwa kwa watumishi wa umma, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Simiyu, Bw. Adili Elinipenda ametoa wito kwa Wakurugenzi kutoa ushirikiano kwa TAKUKURU kuona namna watakavyosaidia pale wanapoletewa barua za kuwafikisha watumishi mahakamani kwa makosa ya rushwa ili kutokuharibu ushahidi.
“Kesi tulizonazo mahakamani nyingi ni za watumishi wa umma na baadhi ya mashahidi tunaowahitaji wanatoka ofisi hizo hizo sasa wakurugenzi wamekuwa hawawasimamishi kazi, kwa hiyo imekuwa ngumu kwa mtumishi kumtolea ushahidi mtumishi mwenzake aliye naye ofisi moja na wakati mwingine ni bosi wake, sasa hapa nafikiri mtaona ni busara gani itumike tunapowatumia barua za kuwafikisha watu mahakamani” alisema Mkuu huyo wa TAKUKURU.
Naye Mratibu wa Utawala Bora kutoka Ofisi ya Rais Ikulu, Bw. Apolinari Tamayamali amesema ni vema Mamlaka za Serikali za Mitaa zikazingatia utaratibu wa sheria unaopaswa kufuatwa wakati mtumishi anapohukumiwa kifungo au faini ili kupata ufumbuzi wa suala hilo.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Utumishi na Utawala wa Halmashauri ya Wilaya ya Itilima, Bi. Pendo Haule kuhusu kusimamishwa kazi kwa mtumishi ambaye ameshtakiwa mahakamani amesema kwa mujibu wa Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2003, sheria imempa nafasi mwajiri ya kumsimamisha kazi au kutomsimamisha kazi mtumishi ambaye ana kesi mahakamani, lakini ikiwa kuwepo kwa mtumishi huyo kazini kunaweza kuharibu ushahidi ni vema sheria ikafuatwa akasimamishwa kazi.
Awali akizungumzia lengo la kuandaa mafunzo kwa kamati za kudhibiti wa Uadilifu, Mratibu wa Utawala Bora kutoka Ofisi ya Rais Ikulu, Bw. Apolinari Tamayamali, amesema ni kuwezesha kamati hizo kupata uelewa wa pamoja juu ya mkakati wa mapambano dhidi ya rushwa awamu ya tatu, namna ya kuandaa mpango kazi na utoaji wa taarifa katika masuala ya mapambano dhidi ya rushwa hapa nchini.
Ameongeza kuwa jithada hizi za kutoa elimu kwa kamati za udhibiti wa uadilifu zimaeanza mwaka 2017, ambapo hadi kufikia mwaka 2018 mikoa takribani 16 imefikiwa na kwa sasa timu ya wataalam iko katika mikoa yote 10 iliyo salia ili kukamilisha mikoa yote 26 ya Tanzania Bara.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI FUNGU KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2019/03/ras-simiyu-awataka-watumishi-simiyu.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa