Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Ndg. Jumanne Sagini ametoa wito kwa viongozi na watumishi mkoani humo kushirikiana na wadau mbalimbali wenye nia njema ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika uboreshaji wa huduma za afya kwa wananchi.
Sagini ameyasema hayo leo katika ufunguzi wa kikao cha kuutambulisha Mradi wa USAID Boresha Afya, kilichofanyika katika Ukumbi wa Kanisa Katoliki Mjini Bariadi.
Amesema Simiyu ni miongoni mwa mikoa saba ambayo Mradi wa USAID Boresha Afya utatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano (2017-2022), hivyo akawataka viongozi na wataalam kushirikiana na wadau hao kuhakikisha mradi huu unasaidia kubadilisha mfumo wa utoaji huduma za afya katika maeneo yaliyobainishwa.
Aidha, amengeza kuwa ujio wa Mradi huu katika Halmashauri zote za Mkoa wa Simiyu uwe ni chachu ya kuhakikisha huduma za Afya zinapatikana kirahisi kwa wananchi wa Mkoa huo.
“Ndugu washiriki nichukue nafasi hii kushukuru mashirika na wadau mbalimbali wanaounga mkono juhudi za Serikali, natoa wito kwa Idara ya Afya Mkoa na wilaya kutoa ushirikiano wa karibu kuhakikisha mradi huu unafanikiwa na unatoa matunda tarajiwa”
Sagini amesema Serikali inafanya juhudi za kukabiliana na viashiria muhimu visivyoridhisha vya Afya ya Uzazi na mtoto ikiwemo kupunguza vifo vya akina mama vitokanavyo na uzazi ambavyo vinafikia 556 kwa kila vizazi hai 100,000 kwa sasa.
“Vifo hivi vinachangiwa na mambo mengi, ikiwemo mahudhurio hafifu ya wajawazito kliniki katika theluthi ya kwanza ya mimba kwa asilimia 24 na wajawazito wanaohudhuria kliniki kwa mahudhurio manne au zaidi kwa asilimia 51” amesema Sagini
Sagini amesisitiza kuwa mafanikio katika suala la kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi halitatatuliwa na sekta ya Afya pekee bali kwa ushirikiano wa sekta zote za maendeleo
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Simiyu, Dkt.Fredrick Mlekwa amesema Mradi huu umekuja katika wakati muafaka ambao mkoa huo unafanya jitihada mbalimbali za kukabiliana na vifo vya akina mama vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto wadogo chini ya miaka mitano.
Naye Dkt.Joseph Masenga kutoka USAID Boresha Afya amesema mradi huo katika mkoa wa Simiyu utajikita katika kuunga mkono juhudi za Serikali katika huduma za uzazi wa mpango, Malaria, Huduma za Afya ya Mtoto, huduma za Uzazi, Lishe na maeneo mengine mtambuka ikiwemo jinsia, heshima na ushirikishwaji wa jamii katika huduma za Afya (ngazi ya jamii).
Kwa upande wake Mratibu wa Mradi wa USAID Boresha Afya wa Mkoa wa Simiyu , Dkt. Charles Suka amesema utambulisho wa mradi huo umefanyika kwa viongozi na watendaji wa mkoa huo ili wawena uelewa wa pamoja ili waweze kutoa mchango katika utengeenzaji wa mapango mkakati wa kupunguza vifo vya mama na mtoto na kuweka mpango wa utekelzaji wa wa mradi kwa miaka mitano.
Mradi wa USAID Boresha Afya Mkoani Simiyu, unatekelezwa kwa ubia wa mashirika ya Jhpiego, Engenderhealth katika mikoa ya Kanda ya Ziwa na Magharibi ambayo ni Simiyu, Mara,Kagera, Kigoma, Shinyanga, Geita na Mwanza katika kipindi cha miaka mitano(2017-2022).
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa