Waziri Mkuu Mstaafu wa Awamu ya nne, Mhe. Mizengo Pinda, amefungua Kongamano la Kilimo Biashara katika Maonesho ya Nanenane Kitaifa mwaka 2019 yanayoendelea katika Viwanja vya Nyakabindi Bariadi Mkoani Simiyu, ambapo amesema kilimo biashara kinaweza kutoa mwongozo wa changamoto ya tija ndogo katika kilimo; ikiwa ni pamoja na matumizi ya kilimo cha umwagiliaji, matumizi ya teknolojia sahihi katika uzalishaji na hifadhi ya mazao.
Mhe. Pinda ameyasema hayo Agosti 06, 2019 mjini Bariadi katika kongamano la Kilimo Biashara lililofanyika wakati wa Maonesho ya Nanenane Kitaifa mwaka 2019 yanayofanyika Kitaifa Kanda ya Ziwa Mashariki Viwanja vya Nyakabindi Bariadi Simiyu.
Mhe. Pinda amesema kuwa ni vyema wakatumia teknolojia za kisasa zilizopo ili waweze kupata tija kwenye kilimo ambacho kina mchango katika pato la Taifa na kubainisha kuwa mchango wake bado ni mdogo kutokana na sababu nyingi ikiwemo mabadiliko ya hali ya hewa hatua inayopelekea kilimo kutokuwa na tija ya kutosha.Ameongeza kuwa hakuna haja kwa wakulima kulima kwa kutegemea mvua ilihali maeneo mengi ya Mikoa ya Kanda ya Ziwa yanazungukwa na ZiwaVictoria lenye maji mengi ambayo yakitumika vizuri wataweza kuzalisha mavuno mengi kwenye eneo dogo kupitia umwagiliaji na teknolojia za kisasa zilizopo.
“niishauri tu Mikoa hii ambayo inazungukwa na Ziwa lenye maji mengi ambayo nchi jirani zinatumia maji hayo kuzalisha mazao kutokana na umwagiliaji badala ya kutegemea mvua; unapotokea ukame unaathiri mazao hayo ipo haja ya kuona umuhimu wa kwenda kwenye kilimo cha umwagiliaji”alisema waziri mkuu mstaafu PindaKwa upande wake Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga amesema sekta ya kilimo ina uwezo wa kuongeza pato la Taifa kwani inachangia kwa asilimia 28.7 huku akibainisha kuwa tija ya uzalishaji kwa wakulima bado ipo chini huku akikisitiza matumizi sahihi ya ardhi na maji hususani kwenye shughuli za umwagiliaji.Ameongeza kuwa licha ya asilimia 65.5 ya Watanzania kujiajiri kwenye sekta ya kilimo moja kwa moja asilimia 66% zinahitajika kwenye viwanda na kwamba zinatakiwa kuboreshwa ili ziweze kufikia angalau 80%.
Katika hatua nyingine Mhe. Hasunga ametoa wito kwa wawekezaji kuwekeza kwenye viwanda vya mafuta kwani Serikali inatumia fedha nyingi kuagiza mafuta nje ya nchi licha ya kuwa mazao mengi yana malighafi ambazo zina uwezo wa kutengeneza mafuta ya kula zipo nchini.“tuna mazao mengi ambayo malighafi zake zina uwezo wa kutengeza mafuta lakini serikali inatumia fedha nyingi kuagiza nje ambapo kwa mwaka ni tani 570,000 huku uwezo wa kuzalisha ukiwa ni tani 250,000 na katika hili tutatumia maamuzi magumu ili tuwekeze kwenye viwanda vya mafuta” alisema waziri Hasunga.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka ameyataka makundi ya wanawake, vijana na waoneshaji kwa ujumla wake kutumia fursa ya uwepo wa Kongamano la Kilimo Biashra kujifunza ili waweze kuongeza ujuzi ambao utaenda sambamba na kutambua mnyororo wa thamani kwenye mazao na shughuli zao za kilimo.
Hata hivyo Mkurugezi wa Mtendaji Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF) Tausi Kida amesema kuwa wakati umefika kwa wakulima kutumia maeneo madogo kuzalisha uzalishaji wenye tija unaoenda sambamba na mazao bora ambayo yatakuwa na uhakika kwenye masoko ya nje.
MWISHO.
kUPATA PICHA ZAIDI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2019/08/waziri-mkuu-mstaafu-pinda-afungua.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa