Naibu Waziri wa Madini Mhe.Stanslaus Nyongo amefanya ziara yake ya kikazi leo Mkoani Simiyu.
Katika ziara hiyo Mhe.Nyongo amekutana na baadhi ya viongozi wa Mkoa wa Simiyu pamoja na watumishi wa Ofisi ya Madini ya Mkoa huo, lengo likiwa ni kuzungumza masuala mbalimbali kuhusu usimamizi wa Sekta ya madini katika Mkoa wa Simiyu, ili kuleta tija kwa wanachi na Taifa kwa ujumla.
Mhe.Nyongo pia amepata fursa ya kutembelea na kuona Jengo la sasa la Ofisi ya Afisa Madini Mkazi na kuahidi kuwa Wizara yake ina mpango wa kujenga jengo la jipya la Ofisi hiyo.
Aidha, amesema atahakikisha tafiti juu ya ubora wa chumvi inayozalishwa wilaya ya Meatu zinafanyika ili kuweza kujua ikiwa inakidhi ubora unaotakiwa kwa matumizi ya binadamu iweze kuongezewa thamani na kutangazwa.
“Tutahakikisha tafiti hizi zinafanyika na mpango wetu ni kwamba zifanyike kwa haraka ili chumvi ya Meatu tuweze kuitangaza, kwa sababu Simiyu tumeshaitangaza vizuri kupitia Chaki sasa tuitangaze tena kwa chumvi yetu” amesisitiza.
Kwa upande wake Afisa Madini Mkazi wa mkoa wa Simiyu, Fabian Mshai amesema wachimbaji wa chumvi wako tayari na wanaomba Mamlaka ya Chakula na Dawa(TFDA) kufanya utafiti kwenye chumvi hiyo na kushauri namna bora ya kufanya chumvi hiyo iwe bora, ili iweze kupata soko zuri ndani na nje ya nchi.
Naye Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Ndg.Jumanne Sagini amesema ni vema Watendaji wa Ofisi ya Madini Mkoa wakasaidiwa kwa kuwezeshwa vitendea kazi pamoja na mahitaji mengine ili waweze kutekeleza vizuri majukumu yao, ikiwa ni pamoja na kuwafikia wachimbaji kwenye maeneo yanayochimbwa madini na Serikali iweze ipate stahili yake.
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa