Naibu Waziri wa Kilimo, Dkt. Mary Mwanjelwa ametoa wito kwa wananchi hapa nchini kupanda miti kwa wingi ili kuboresha mazingira, kutunza uoto wa asili, kuwa na uhakika wa mvua na kuepukana na ukame.
Ushauri huo ameutoa katika Uwanja wa Nyakabindi katika Maonesho ya Kilimo na Sherehe ya Wakulima Nane nane wakati wa zoezi la kupanda miti, lililofanyika leo Agosti 02, 2018
Mwanjelwa amesema ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi zoezi la upandaji hapa nchini linapaswa kuwa endelevu kwa wananchi.
"Tumepanda miti hii kwenye Uwanja wa Nanenane Nyakabindi Bariadi ni sehemu ya uhamasishaji kwa viongozi na wananchi wote kupanda miti, nitoe rai kwa viongozi na wananchi wote mkoani Simiyu kuendeleza zoezi hili ili maana tukipanda miti tunaboresha mazingira, tunapata mvua ya uhakika, kuboresha uoto wa asili hata mifugo yetu inapata malisho" alisema.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Profesa Elisante Ole Gabriel amesema upandaji wa miti una uhusiano Mkubwa na mifugo katika Ustawi wa malisho, huku akitoa wito kwa uongozi wa Mkoa wa Simiyu kuendeleza zoezi hili ili kumuunga mkono Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania za kuifanya Tanzania kuwa ya kijani.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu , Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga amesema mkoa unatarajia kupanda miti zaidi ya milioni tatu .
Katika hatua nyingine Naibu waziri wa Kilimo ametembelea Banda la Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kulipongeza jesho hilo kwa namna linavyopambana na majanga ya moto na kusisitiza kuendelea kutoa elimu ya mara kwa mara kwa wananchi juu ya kukabiliana na majanga ya moto.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI KUHUSU HABARI HII FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2018/08/naibu-waziri-mwanjelwa-ahimiza-wananchi.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa