Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Omary Mgumba amemuagiza Mhandisi wa Umwagiliaji Tume ya Umwagiliaji Kanda ya Mwanza, Ebenezer Kombe kufanya tathmini katika Skimu ya Umwagiliaji ya Kinamwigulu Wilayani Maswa, kuona kama kuna uwezekano wa kujenga bwawa, ili Serikali iweke mipango ya kujenga bwawa hilo kuwawezesha wananchi kulima bila kutegemea mvua.
Mhe. Mgumba ameyasema hayo wakati alipotembelea eneo la skimu hiyo na kupokea ombi kutoka kwa wananchi la kuomba kujengewa bwawa na kuboreshewa mundombinu mingine, wakati akiwa katika ziara yake ya kukagua shughuli za kilimo na miradi ya umwagiliaji wilayani Maswa Machi 07, 2019.
Amesema mara baada ya kupokea taarifa ya tathmini itakayofanywa na wataalam wa umwagiliaji ikionekana katika eneo hilo Bwawa linaweza kujengwa Serikali itahakikisha inaweka katika Mpango wa bajeti fedha kwa ajili ya bwawa hilo, ili kukidhi haja ya wananchi ya kulima kwa umwagilia kwa lengo la kujikwamua kiuchumi.
“Mhandisi wa Umwagiliaji wa Kanda ni vizuri ukaja hapa na wataalam mkafanya tathmini kuona je inawezekana kujenga mabwawa hapa, baada ya tathmini tukishafahamu kuwa panafaa kujenga bwawa ndiyo tuweke katika mpango wa bajeti” alisema Mgumba.
Kwa uapnde wao Wananchi hao wamesema wakijengewa bwawa na kuboreshewa miundobinu umwagiliaji watakuwa na uhakika wa kulima bila kutegemea mvua angalau mara mbili kwa mwaka, ambapo pia wameomba kuwezeshwa zana bora za kilimo.
“Tunaiomba Serikali itujengee bwawa kuendeleza kilimo cha umwagiliaji ili kusudi tuwe tunalima mara mbili kwa mwaka badala ya kutegemea mvua peke yake” alisema mkulima wa Kinamwigulu
“Pamoja na ombi la kutujengea bwawa litakalotusaidia kulima misimu miwili kwa mwaka tunaomba pia Serikali ituletee mikopo ya matrekta ili tuweze kulima maeneo makubwa zaidi” alisema Charles Hege mkulima wa Kinamwigulu
Katika hatua nyingine Mhe. mgumba amesisitiza suala la Halmashauri kutenga asilimia 20 ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya kuendeleza shughuli za uzalishaji ikiwemo kilimo kwa kuwa zina mchango mkubwa katika mapato ya Halmashauri, badala ya kuwekeza fedha nyingi kwenye miradi ya kutoa huduma pekee.
Awali akitoa taarifa ya Wilaya, Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dkt. Seif Shekalaghe ameiomba Bodi ya Pamba kuwashirikisha viongozi wa Wilaya na Halmashauri katika kuandaa mwongozo wa ununuzi wa pamba, ili waweze kupata nafasi ya kutoa maoni yao kwa kuwa ni wadau muhimu na wasimamizi wakubwa katika uzalishaji wa zao hilo.
Akiwa Wilayani Maswa, Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Omary Mgumba ametembelea skimu ya umwagiliaji ya Kinamwigulu na shamba la pamba lenye ukubwa wa ekari tano linalomikiliwa na kikundi cha wanawake kiitwacho Upendo, kilichopo Kijiji cha Busamda.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2019/03/naibu-waziri-mgumba-aagiza-tume-ya.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa