Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana na Ajira, Mhe.Anthony Mavunde ametoa wito kwa wanafunzi wa kidato cha sita Mkoani Simiyu kutokubali mtu yeyote kufifisha wala kukatisha ndoto zao badala yake wasome kwa bidii.
Mavunde ametoa wito huo wakati akizungumza na wanafunzi zaidi ya 1000 kutoka shule kumi na mbili za sekondari za kidato cha sita walioko katika kambi ya kitaaluma, shule ya sekondari ya wasichana Maswa.
Mavunde amesema Taifa lolote duniani linajengwa na vijana na hasa vijana wasomi hivyo wanapaswa kusoma kwa bidii, ili wasiwaangushe, wazazi na jamii inayowazunguka ambayo inawategemea, huku akipongeza uongozi wa mkoa kuanzisha kambi za kitaaluma ambazo zimeoneka kuusaidia mkoa kupanda katika ufaulu.
“wanafunzi msikubali ndoto zenu zikatishwe, someni kwa bidii mfikie ndoto zenu, Taifa wazazi na jamii inayowazunguka inawategemea, msiwaangushe viongozi wenu waliofanya mkawa hapa, Mkoa wa Simiyu ndio umetuonesha kuwa kumbe kambi za kitaaluma zinawezekana” alisema Mhe. Mavunde.
Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amewapongeza walimu wote kwa kazi nzuri wanayoifanya na kueleza lengo la kuanzishwa kambi za kitaaluma ambazo amesema zimeonekana kuwa na mwamko mkubwa kwa wanafunzi.
“Sisi tulitafakari watoto wetu wanatoka kwenye mazingira ya kawaida tukajiuliza kwa nini wasikae kwenye madarasa yaliyo na sakafu na dari safi wakasoma, tumejaribu kwenye shule za O’level (kidato cha nne) tumeona mwamko wa watoto kusoma” alisema Mhe. Mtaka.
Kwa upande wao viongozi na wadau mbalimbali wa elimu waliowatembelea wanafunzi hao pia walipata nafasi ya kuwausia wanafunzi hao wa kidato cha sita na kuwasisitiza juu ya umuhimu wa kufanya bidii ili kufikia malengo yao.
“ Tunajadiliana hapa ili kuwa na uelewa wa pamoja, ninataka kuwaambia kuwa hakuna mafanikio yanayokuja kwa bahati mbaya iwe katika masomo hata katika maisha,” alisema Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisha.
“Mnaweza kutimiza ndoto zenu bila kujali mahali mtu anapotoka, najua wengi wetu hapa tumetoka katika familia za kawaida, tumesoma shule za kawaida kabisa lakini tulifanikiwa, hata ninyi mnaweza ni suala la kuamua tu” alisema Happiness Lugiko Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki.
Naye Askofu wa Kanisa la Waadventista Wasabato Jimbo Kuu la kusini, Mch. Mark Malekana amesema ili wanafuzi hao waweze kufikia ndoto zao wanapaswa kuwa na dhamira ya kushinda, wasome kwa bidii, wawe na nidhamu, washinde hofu wanapokuwa kwenye mitihani na wamwamini Mungu.
Mwanafunzi Kelista Joseph kutoka shule ya sekondari Itilima amesema maswali mbalimbali ambayo wamekuwa wakiyafanyia kazi yatawasaidiana mwishowe watafanya vizuri na wanaamini kama walivyoahidi toka siku ya kwanza ya kambi kwamba watapata ‘Division One’ wote.
Kambi ya Kitaaluma kwa wanafunzi wa Kidato cha Sita mwaka 2019 Mkoani Simiyu inatarajiwa kufungwa rasmi Aprili 28, 2019 na baadaye wanafunzi watarejea katika shule zao kwa ajili ya maandalizi ya Mtihani wa Taifa unaotarajia kuanza Mei 06, 2019.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI KUHUSU HABARI HII FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:https://simiyuregion.blogspot.com/2019/04/naibu-waziri-mavunde-awataka-kidato-cha.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa