Naibu Waziri wa Madini, Mhe. Stanslaus Nyongo ametoa muda wa siku moja kwa Mkandarasi SUMA JKT anayejenga Jengo la Kituo cha Umahiri Simiyu kuamilisha sehemu ya Jengo hilo iliyopangwa kutumika kama Soko la Madini la Mkoa.
Nyongo ameyasema hayo Mei 02, 2019 wakati alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo ambalo sehemu litatumika kama kituo cha umahiri na sehemu kama Soko la Madini la Mkoa.
“ Kwa mkoa wa Simiyu tumeona hapa tunaweza kupatumia kwa kuanzia kwenye soko la madini, nimeshatoa maagizo kuwa jengo hili walimalizie mara moja, ili waweze kutoa sehemu ambayo itatumika kwa ajili ya soko la madini na kufikia kesho jioni tunataka jengo hili lianze kutumika kama soko la Madini “ amesema Nyongo.
Aidha, Nyongo amesema anatumia fursa hiyo kuwajulisha wachimbaji wadogo wadogo wa madini kuwa Simiyu kutakuwa na jengo ambalo litatumika kununua na kuuza madini.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema kama mkoa wamejipanga vizuri katika soko la madini, huku akiwakaribisha wafanyabiashara wa madini kutoka mkoa wa Simiyu na mikoa jirani kufika katika kituo hicho ambacho amesema kitakuwa kituo bora chenye uhakika wa kufanya biashara hapa nchini.
Mtaka ameongeza kuwa kituo hicho ambacho kitafunguliwa rasmi wiki ijayo kitatoa fursa kwa Watanzania kuanza kuangalia ufanyaji wa biashara katika eneo la madini kwa njia ambazo ni halali, akatoa wito kwa wafanyabiashara wa mkoa wa Simiyu pamoja na kuwekeza biashara katika kilimo, mifugo na viwanda wawekeze pia katika biashara ya madini.
Naye Sajenti Emmanuel Igogo kutoka SUMA JKT amesema agizo la Naibu Waziri la kukamilisha sehemu ya Jengo la Kituo ca Umahiri ambayo itatumika kama soko la madini (Kituo cha kuuzia madini) litatekelezwa kama lilivyoagizwa.
“ Tutatekeleza agizo la Mhe. Naibu Waziri tutaanza leo kulifanyika kazi na kwa kuwa kazi hii haikuwepo kwenye mkataba wetu wa awali nitawasiliana na viongozi wangu na tutakamilisha” alisema Sajenti Igogo.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2019/05/naibu-waziri-madini-atoa-siku-moja-kwa.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa