Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya watu wenye ulemavu, Mhe.Stella Ikupa ametoa wito kwa viongozi wa vyama vya watu wenye ulemavu, kuwahamasisha wanachama wao kujiunga na mfuko wa afya ya jamii (CHF )ulioboreshwa ili waweze kupata uhakika wa matibabu.
IKUPA ametoa wito huo wilayani Itilima katika ziara yake wakati akizungumza na viongozi wa Wilaya, Viongozi wa Vyama vya wenye ulemavu na baadhi ya wenye ulemavu wenyewe wakati wa ziara yake wilayani humo Februari 25, 2019, ambayo ililenga kukagua utekelezaji wa maelekezo ya Serikali ikiwa ni pamoja na mradi wa Kitalu nyumba na masuala mbalimbali yahusuyo wenye walemavu.
Amesema ni vema viongozi wa vyama na wenye ulemavu wakapena taarifa na kuhamasishani kujiunga na mfuko wa Afya ya Jamii(CHF) ulioboreshwa, ili wapewe vitambulisho waweze kutibiwa kirahisi.
“Mkijiunga na CHF iliyoboreshwa mkapata kadi mtakuwa na uwezo wa kutibiwa muda wowote, kwa hiyo peaneni hizo taarifa mjiunge watu mnaofahamiana muweze kupewa hivyo vitambulisho mpate kutibiwa kirahisi wakati tukiwa tunasubiri ile bima ya afya kwa kila Mtanzania” alisema Mhe. Ikupa.
Katika hatua nyingine amewaagiza maafisa Ustawi wa jamii na maendeleo ya jamii kutoa elimu vijijini kwa watu wenye ulemavu kuhusiana na uundwaji wa vikundi na namna ya kutekeleza miradi mbalimbali.
Mkuu wa Wilaya ya Itilima,Mhe. Benson Kilangi akizungumzia utekelezaji wa mradi wa kitalu nyumba amesema katika awamu ya kwanza jumla ya vijana 20 wamepata mafunzo ya utengenezaji wa vitalu nyumba na kufundishwa stadi mbalimbali za kuendesha kilimo biashara na kuongeza mnyororo wa thamani.
Naye Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Festo Kiswaga amesema miradi ya vitalu katika Mkoa wa Simiyu itatekelezwa kwa viwango na kwa malengo yaliyokusudiwa, huku akibainisha kuwa vitasaidia kuongeza kipato kwa wananchi katika mkoa na kuwa sehemu ya wananchi kujifunza kilimo bora.
Kwa upande wao viongozi pamoja na watu wenye ulemavu walioshiriki katika ziara hiyo wamemwomba Mhe. Naibu Waziri kushughulikia baadhi ya changamoto zinazowakabili katika maeneo yao.
“Ninaomba Serikali itusaidie tuweze kupata wakalimani wa lugha ya alama ili na sisi walemavu wa kusikia tuweze kupata ujumbe unaokuwa unawasilishwa na viongozi wetu kwenye mikutano na ziara kama hii ya leo hii itatusaidia sana” alisema Mhandi Ntobi Mwenyekiti wa Chama cha Walemavu wasiosikia Mkoa wa Simiyu.
“NaombaWataalam waje watutembelee kwenye vijiji vyetu na kwenye vyama vyetu watusaidie kutupa elimu ya namna ya kuunda vikundi na namna ya kufanya shughuli zinazoweza kutuongezea kipato” Bw. Seni Jitabo mlemavu wa viungo Mkazi wa Zagayu wilayani Itilima.
Naibu Waziri Ikupa, anaendelea na ziara yake Mkoani Simiyu ambayo itahitimishwa 27 Februari 2019, akiwa wilayani Itilima Naibu waziri ametembelea kitalu nyumba kilichopo Lagangabilili na kituo cha maarifa ya jamii Kanadi, ambako amejionea shughuli mbalimbali za uzalishaji zinazofanywa na vijana.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2019/02/naibu-waziri-ikupa-atoa-wito-kwa-wenye.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa