Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Bw. Amon Mpanju ameupongeza uongozi wa Mkoa wa Simiyu kwa namna unavyojishughulisha na masuala ya watu wenye ulemavu na kukubali kuwa mwenyeji wa Siku ya watu wenye Ulemavu Kitaifa inayotarajiwa kufanyika Desemba 03 mwaka huu mjini Bariadi.
Mpanjo ameyasema hapo alipomtembelea Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Anthony Mtaka ofisini kwake leo Juni 25 mara baada ya kufungua semina elekezi kuhusu Sheria ya Msaada wa Kisheria na kanuni zake kwa wasaidizi wa msaada wa kisheria mkoani humo.
"Ninawapongeza sana kwa kuwajali watu wenye ulemavu, mmekuwa wenyeji wa siku ya watu wenye ualbino mwaka huu, mmekubali kuwa wenyeji wa siku ya watu wenye ulemavu mwaka uliopita na mwaka huu tena mwezi Desemba, binafsi nawashukuru sana Simiyu" alisema.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema maadhimisho ya siku ya watu wenye ulemavu mwaka 2017 yaliyofanyika mkoani humo, lakini Simiyu imekubali kuwa mwenyeji tena kwa mwaka 2018 ili kujipanga upya na kuyafanya maadhimisho hayo kuwa ya tofauti.
"Mwaka jana tulifanya maadhimisho ya watu wenye ulemavu Kitaifa hapa Simiyu lakini nilitamani tukio hili lifanyike katika ukubwa wake, kwa dhamira hii hii mwaka 2018 tumekubali kuwa wenyeji ili tuyaandae maadhimisho haya tena kama tukio kubwa ambalo litahusisha watu wengi na kufanyika kwa uzito wake tofauti na mwaka jana" alisema Mtaka.
Mtaka amesema ameongea na viongozi mbalimbali wa ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kuona uwezekano kwa watu wenye ulemavu kufanya shughuli mbalimbali na kuonesha kazi mbalimbali wanazofanya, wiki moja kabla ya kilele ambacho kitakuwa Desemba 03, 2018.
Aidha, amesema pamoja na kuweka mipango ya watu wenye ulemavu kuonesha kazi zao kabla ya kilele pia upo mpango wa kuwashirikisha katika michezo mbalimbali ili waweze kuonesha vipaji vyao katika michezo.
Ameongeza kuwa dhamira ya Mkoa wa Simiyu pia ni kuwa kongamano kabla ya kilele ambalo litatoa fursa ya kufanya mijadala kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo masuala kitaaluma, ujasiriamali, stadi za maisha na mengine ambayo yatawaleta pamoja watu wenye ulemavu kutoka maeneo tofauti.
Mgeni rasmi katika siku ya watu wenye ulemavu ambayo inatarajiwa kuadhimishwa Kitaifa Mjini Bariadi Mkoani Simiyu, anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa.
MWISHO
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa