Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu, Mhe. Enock Yakobo ameishauri Serikali kutoa kipaumbele kwa wilaya mpya za Busega na Itilima mkoani humo, katika Ujenzi wa Ofisi na Nyumba za Watumishi ili watumishi waweze kufanya kazi katika mazingira mazuri.
Mhe. Yakobo ameyasema hayo leo alipotembelea na kuona Ujenzi wa Jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Busega ambalo mpaka kukamilika kwake litagharimu shilingi bilioni 4.6 , wakati wa Ziara ya Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa ya kukagua Utekelezaji wa Ilani ya CCM wilayani humo.
“Ingekuwa vizuri Ofisi na nyumba za watumishi zipatikane maana Busega imeshajitegemea, kama mkoa tuwe na kaulimbiu hiyo kuwa wilaya hizi mpya ziangaliwe; eneo hili ni changa linapaswa kuendelezwa ili watumishi wa hapa nao wafurahie utumishi wao”alisema Mhe.Yakobo
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka amesema Serikali ya Mkoa kwa kushirikiana na Wakurugenzi wa Halmashauri waliwasilisha suala hilo kwa Kamati ya Bunge na kuomba mkoa wa Simiyu kwa kuwa ni mpya uangaliwe sana kwenye mahitaji muhimu hususani yanayowagusa watumishi ikiwemo makazi.
“Ningependa kuwaomba Mwenyekiti wa CCM mkoa na Mjumbe wa NEC mlibebe jambo hili kama agenda ya Mkoa, sisi kama Serikali tulienda pamoja na Wakurugenzi kwenye Kamati ya Bunge, tukaomba kama Mkoa mpya waangalie mahitaji ya msingi hasa kwa watumishi, majengo yote haya tumeyaombea fedha na majengo ya Mkoa pia tumeyaombea fedha” alisema Mtaka.
Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Ndg. Jumanne Sagini amesema Serikali imeshajenga nyumba nne (04) kwa ajili ya watumishi wa Halmasahuri ya Wilaya ya Busega na mpango wa kuendelea kupata fedha kwa ajili ya kujenga nyumba zilizobaki unaendelea.
Aidha, Sagini amesema Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kukamilisha jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Busega, Ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Busega pamoja makazi yake
Katika hatua nyingine Sagini amewataarifu wajumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Simiyu kuwa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo na kukamilisha ujenzi wa Nyumba za Viongozi wa Mkoa zimetengwa.
Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa ikiongozwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa Mhe.Enock Yakobo pamoja na kukagua jengo la Halmashauri wilayani Busega ilikagua Miradi mingine ya maendeleo katika Sekta ya Maji, Elimu na Afya.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI KUHUSU HABARI HII FUNGUA HAPA:-https://simiyuregion.blogspot.com/2018/04/mwenyekiti-wa-ccm-simiyu-aishauri.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa