Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania, Bw. Masanja Kadogosa amewataka vijana hapa nchini kuwa ndoto ili waweze kuona na kuzifikia fursa mbalimbali zilizopo na kukuza Uchumi wao na Taifa kwa ujumla, kupitia uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano katika Sekta mbalimbali.
Kadogosa ameyasema hayo Septemba 14, 2018 wakati akizungumza na Vijana wa Mkoa wa Simiyu, katika Kongamano la Vijana wa Mkoa wa huo lililoandaliwa na Asasi ya Wanafunzi wa Vyuo Vikuu na Waliohitimu wanaotoka mkoa wa Simiyu- Simiyu University Students and Associates Association (SUSAA), lililofanyika Mjini Bariadi .
Amesema Serikali imewekeza fedha nyingi katika sekta ya viwanda, nishati, ujenzi wa miundombinu kama reli ya kisasa, barabara na miundombinu ya usafiri wa anga na majini kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu, hivyo vinana wanapaswa kuwa na ndoto zitakazowawezesha kuziona fursa ili wajikwamue kiuchumi.
“Ni jambo muhimu sana kwa vijana kuwa na ndoto kwa sababu wakiwa na ndoto wataona fursa, ndoto zitawasaidia kufikiria namna ya kujiwekea malengo; Serikali imewekeza kwenye vitu vingi sana na kutengeneza mazingira wezeshi, ni wakati wao sasa vijana kutambua nafasi yao katika kuzitumia fursa hizo” alisema
Aidha, Kadogosa ameshauri makongamano ya Vijana kama lililofanyika Mkoani Simiyu yafanyike pia katika mikoa mingine na akatoa wito kwa Viongozi na watu mbalimbali wawe tayari kutoa elimu, ushauri, uzoefu ili kuwajengea uwezo vijana hapa nchini.
Awali akifungua Kongamano hilo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka, Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga amewataka vijana wa mkoa huo kufuata nyayo za wazazi wao katika kuweka jitihada kwenye kilimo ambapo uzalishaji wa pamba mwaka 2018 umefikia takribani kilo milioni 140 kutoka kilo 70 za msimu uliopita.
Aidha, Kiswaga amesema vijana hao wajiandae pia katika uwekezaji kwenye viwanda “Sasa hivi Serikali inaenda kwenye viwanda na hapa naviona viwanda vingi sana hapa naviona viwanda viwanda vya nguo, naviona viwanda vidogo vingi sana kutoka kwenu, kwa hiyo tujiandae katika kuhakikisha mkoa huu tunawekeza na wawekezaji ni sisi tuliopo kwenye kongamano hili”.
Kwa upande wake Waziri wa Uvuvi na Mifugo, Mhe. Luhaga Mpina, ambaye alikuwa miongoni mwa watoa mada katika kongamano hilo, amewataka vijana hususani wahitimu wa Vyuo Vikuu kutumia fursa zilizopo hapa nchini hususani katika sekta ya Kilimo, Uvuvi na Ufugaji kujiajiri badala ya kusubiri kuajiriwa.
Awali akisoma risala kwa niaba ya Vijana wa Mkoa wa Simiyu na Viongozi wa SUSAA, Mwenyekiti wa SUSAA Kanda ya Mashariki, Bw. Musa Joseph amesema lengo kuu la kongamano hilo ni kuwakutanisha vijana pamoja ili kueleweshana juu ya dhana ya uchumi wa viwanda nchini na namna kila kijana anavyoweza kushiriki kwa vitendo katika eneo lake.
Nao baadhi ya Vijana wakiongelea Kongamano hilo wamesema kuwa limewasaidia fursa kubwa kwao ya wao kupata elimu, ujuzi, na kugundua fursa za uwekezaji na kujiajiri wenyewe badala ya kusubiri kuajiriwa.
“ Kongamano hili limetusaidia sana sisi vijana kugundua fursa nyingi za kuwekeza, kujiajiri ambazo vijana wengi bado hawajaweza kuzitumia katika kuhakikisha wanajiletea maendeleo, naamini kupitia elimu tuliyoipata leo tutazitumia vizuri fursa zilizopo, ili tujiletee maendeleo” alisema Emmanuel Lyaganda
Kongamano hili lilihusisha vijana kutoka maeneo tofauti wanaojishughulisha na shughuli mbalimbali na limeandaliwa na Asasi ya Vijana walioko Vyuo Vikuu na waliohitimu ambao ni wakazi wa mkoa wa Simiyu- Simiyu University Students and Associates Association(SUSAA), likiwa na Kauli mbiu isemayo “ VIJANA NA UWEKEZAJI KATIKA KUELEKEA UCHUMI WA VIWANDA TANZANIA”.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI KUHUSU HABARI HII FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2018/09/mkurugenzi-trl-awataka-vijana-kuw-na.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa