Mkoa wa Simiyu umejiwekea mikakati mbalimbali kuboresha hali ya lishe mkoani humo ikiwa ni pamoja na kukabiliana na tatizo la utapiamlo kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano.
Hayo yamesemwa na Mratibu wa Lishe Mkoa wa Simiyu, Dkt. Chacha Magige katika kikao cha kamati ya lishe kilichofanyika katika Ukumbi wa Hospitali Teule ya Mkoa, Mjini Bariadi.
Chacha amesema elimu inatolewa kwa wananchi hususani akina mama wajawazito na wanaonyonyesha juu ya umuhimu kula vyakula vinavyotokana na makundi yote matano na kuhakikisha kuwa elimu ya lishe kwa akina mama inatolewa katika kliniki ya mama na mtoto na vidonge vya madini Chuma na Folic Acid vinatolewa
Aidha, amesema elimu ya uandaaji na uhifadhi wa vyakula vinavyotoa virutubishi vya kutosha; mfano, ufundikaji na uchachushaji wa vyakula inatolewa na mpango mkakati wa lishe wa Mkoa utakaowezesha kutambua changamoto mbalimbali za lishe, na kuzipatia ufumbuzi, na hatimaye kubadilisha hali ya lishe ilivyo unakamilishwa kwa wakati.
Ameongeza kuwa Idara ya Afya itatumia maonesho ya NaneNane yatakayofanyika Kitaifa Mkoani Simiyu kuelimisha jamii juu ya wakina mama kuwanyonyesha watoto maziwa ya mama mara tu baada ya kuzaliwa, kunyonyesha watoto maziwa ya mama pekee kwa muda wa miezi sita ya mwanzo na baada ya hapo kuwaanzishia vyakula vya nyongeza.
Pamoja na elimu ya masuala ya lishe, Chacha amesema elimu juu ya uzazi wa mpango inahitajika kwa wanachi ili kuwasaidia kupata uelewa wa umuhimu wa kuwa na idadi ya watoto watakaoweza kuwahudumia kwa mahitaji ya muhimu ikiwepo chakula bora.
Mwakilishi wa Shirika la CUAMM Bw. Zacharia Msumari amesema shirika hilo limekuwa likitoa tiba ya vyakula (tiba lishe) kwa watoto wenye utapiamlo katika baadhi ya vituo vya kutolea huduma za afya mkoani humo na kuwawezesha baadhi yao kuwa katika hali nzuri.
Ameongeza kuwa shirika hilo pia imekuwa likitoa elimu kwa watoa huduma katika vituo vya kutolea huduma za afya ili nao waweze kuelimisha wazazi na walezi namna ya kukabiliana na utapiamlo kwa kuwalisha watoto vyakula vya makundi yote matano ambavyo vinapatikana katika maeneo yao ili kuimarisha afya zao.
Awali akifungua kikao hicho Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Mhandisi. Mashaka Luhamba ametoa wito kwa wadau wa afya kuendelea kutoa elimu katika jamii juu ya uandaaji wa vyakula katika familia ambavyo vinajumuisha makundi yote matano ya vyakula , kutokana na mkoa wa Simiyu kuzalisha aina mbalimbali za vyakula.
MWISHO
Baadhi ya wadau wa afya na wajumbe wa Kamati ya Lishe ya Mkoa wa Simiyu, wakimsikiliza Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Mhandisi. Mashaka Luhamba katika Kikao cha Kamati hiyo kilichofanyika Mjini Bariadi.
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa