Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka ametoa wito kwa jamii kupiga viya mila na desturi zinazochangia watu kutotumia vyoo na kusisitiza kila kaya ione umuhimu wa kuwa na choo bora, ikiwa ni njia ya kuboresha afya na usafi wa mazingira na kuondokana na hatari ya magonjwa ya mlipuko ikiwemo kipindupindu.
Mtaka ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Usichukulie Poa Nyumba Ni Choo ambao umefanyika Agosti 20, 2019 Mjini Bariadi ambapo amesema ni vema mila hizo zikapigwa vita ili jamii iweze kurudi kwenye msingi.
“Kwenye culture(tamaduni) zetu zipo sababu kwa nini baadhi ya watu walikuwa hawatumii vyoo ambazo ni sababu za kitamaduni, kwamba baba mkwe hawezi kuchangia choo na mke wa kijana wake, kwa hiyo ilikuwa hata ukijenga choo kwa baadhi ya kaya huko nyuma bado kulikuwa na upinzani wa watumiaji”
“Unakuta kuna choo kwenye kaya Fulani lakini bado wanajamii wa hiyo kaya wanaenda kujisiri porini, huu ni utamaduni ambao ni lazima tuufanyie kampeni kama tulivyofanya kampeni za kukataa mambo mengine kama ukeketaji ili jamii zetu zirudi kwenye msingi, katika mkoa wetu kufikia mwezi Novemba, 2019 kila kaya itakuwa na choo bora na kinachotumika” alisema Mtaka.
Aidha, Mtaka amesema anaiunga mkono kwa asilimia 100 Kampeni ya Usichukulie Poa Nyumba Ni Choo kwa kuwa ni kampeni inayolisaidia Taifa katika usafi wa mazingira na kubainisha kuwa itakapofika mwezi Novemba 2019 kila kaya katika Mkoa wa Simiyu itakuwa na choo bora kinachotumika.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini amesema Mkoa wa Simiyu umetajwa kuwa na kaya 215,316 ambapo kati ya hizo zenye vyoo ni 208,856 sawa na asilimia 97 na zenye vyoo bora zikiwa ni 97,536 sawa na asilimia 46.7.
Naye Mratibu wa Kampeni ya Taifa ya Usafi wa Mazingira kutoka Wizara ya Afya Anyitike Mwakitalima amesema kampeni hii inafanyika kwa lengo la kusaidia uboreshaji wa afya nchini kwa sababu magonjwa mengi yanatokana na uchafu na njia moja wapo ya kukabili uchafu ni matumizi wa vyoo bora na unawaji wa mikono kwa maji safi, salama na sabuni.
Amesema Serikali imeendelea kutoa elimu katika jamii kuhusiana na matumizi na ujenzi wa vyoo bora katika ngazi ya kaya na taasisi na tayari mikoa tisa imefikiwa, mkoa wa Simiyu ukiwa mkoa wa kumi ambapo amesema lengo ni kuifikia mikoa yote 26 kabla ya Juni 2020
Kampeni ya Usichukulie Poa Nyumba Ni Choo itafanyika kwa takribani siku 20 katika Halmashauri zote sita za Mkoa wa Simiyu
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2019/08/mila-zinazochangia-jamii-kutotumia-vyoo.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa