Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (SENAPA), William Mwakilema amesema Uwanja wa Ndege Simiyu unaotarajia kujengwa Eneo la Igegu wilayani Bariadi utakapokamilika utaongeza huduma za Utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Mwakilema ameyasema hayo wakati ziara ya Balozi wa Indonesia hapa nchini , Prof.Dkt. Ratlan Pardede na Viongozi wa Mkoa wa Simiyu katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti Mei 16 ili kujionea wanyama na vivutio mbalimbali vya utalii katika hifadhi hiyo.
Amesema Hifadhi ya Serengeti ina uwanja ambao unaowezesha ndege ndogo kutua hivyo, ujenzi wa uwanja wa Simiyu utakaowezesha ndege kubwa kutua itakuwa ni nyongeza ya huduma, ambapo ndege kubwa zitakapotua Simiyu watalii ambao hawawezi kutembea mwendo mrefu kwa kutumia magari, watachukuliwa na ndege ndogo kutoka Simiyu na kupelekwa Seronera(Serengeti).
Ameongeza kuwa, kuwepo kwa uwanja huo kutasaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha huduma za Utalii, ambapo wafanyabiashara wengi wa huduma za Utalii watavutiwa kuwekeza mkoani Simiyu kwa ajili kutoa huduma kwa wageni watakaotua uwanjani hapo na wanaoenda kufanya utalii Serengeti.
Aidha, Mwakilema amesema Mamlaka ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti inaendelea kushirikiana na Mkoa wa Simiyu kuhakikisha kuwa rasilimali zote ndani ya hifadhi ziko salama na zinaendelea kutunzwa ili Taifa liweze kunufaika kiuchumi kupitia utalii.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema Mpango wa Mkoa huo ni kufikisha kwa wepesi huduma za Utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti hivyo mkoa umepanga kujenga uwanja huo wa ndege katika Eneo la Igegu wilayani Bariadi ambalo liko karibu kabisa na Hifadhi hiyo.
“Tumepanga kujenga Uwanja wa Ndege pale Igegu ili kufikisha huduma za utalii kwa wepesi katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na mwaka huu wa fedha 208/2019 tumetengewa fedha kwa ajili ya ujenzi wa uwanja huo utakaokuwa na ukubwa wa kilometa 2.5, pia sisi kama mkoa tutahakikisha tunafungua malango yote ya watalii kuja kwenye vivutio vyetu” alisema Mtaka
“Tunapokamilisha miundombinu ya barabara ya Lamadi-Bariadi-Maswa-Mwigumbi ni pamoja na kuona namna tutakavyounganisha ufunguaji wa barabara zitakazowezesha watu kwenda kwenye hoteli zote za kitalii zilizojengwa ndani ya hifadhi hasa zilizo katika eneo letu, ili huduma za utalii zirahisishwe” alisisitiza.
Kwa upande wake Balozi wa Indonesia nchini Tanzania, Prof. Dkt. Ratlan Pardede baada ya kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti amesema atazungumza na Wafanyabiashara wa Indonesia na kuwaalika kuwekeza katika Sekta ya Utalii nchini Tanzania hususani Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, huku akisisitiza kutoa wito kwa wananchi wa Indonesia kutembelea Hifadhi ya Serengeti ili kuja kujionea vivutio mbalimbali vya utalii.
Balozi wa Indonesia, Prof. Dkt. Ratlan Pardede amehitimisha ziara yake kikazi mkoani Simiyu ambapo ameahidi kuimarisha ushirikiano kati ya Indonesia na Tanzania na hasa Mkoa wa Simiyu katika masuala ya kilimo na biashara ya zao la pamba, uwekezaji wa viwanda vya nguo, bidhaa za ngozi na mbolea pamoja na utalii.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2018/05/mhifadhi-mkuu-serengeti-uwanja-wa-ndege.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa