Uongozi wa mkoa wa Simiyu umetoa siku saba kwa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Bariadi na Ofisi ya Madini Mkoa wa Simiyu kupitia malalamiko na hoja zote za wachimbaji wadogo, wamiliki wa mashamba na wadau wengine katika mgodi wa dhahabu wa Bulambaka wilayani Bariadi na kuhakikisha shughuli za uchimbaji wa madini unafanyika kwa mujibu wa sheria.
Hayo yameelezwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bi. Miriam Mmbaga mara baada ya kiongozi huyo na viongozi wengine wa mkoa kuzungumza na wananchi hao waliofika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Aprili 08, 2021 Mjini Bariadi ili kupata ufumbuzi wa malalamiko yao.
“ Ofisi ya mkuu wa Mkoa wa Simiyu imepokea wachimbaji na wadau mbalimbali wanaofanya kazi katika mgodi wa Bulumbaka na kuwasikiliza baada ya kutoka kwa Mkuu wa Wilaya; hoja za wachimbaji ni pamoja na wao kutokubaliana na utaratibu wa utoaji leseni kwa kikundi kilichopewa leseni kufanya kazi katika eneo lile, ambapo baadhi ya wanakikundi wamedai kuwa hawakitambua kwa kuwa hawakushirikishwa,”
“Baada ya kuwasiliza pamoja na hoja nyingine tumeona hili suala bado liko ndani ya uwezo wa ofisi ya Mkuu wa Wilaya hivyo nimetoa siku saba kwa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na ofisi ya madini mkoa wa Simiyu, wapitie hoja zote na kutoa ushauri na kufanyia kazi yale yote wanayoweza kuyafanyia kazi kwenye ngazi yao kuhakikisha uchimbaji madini ufanyike kwa mujibu wa sheria,” alisema Mmbaga.
Nao baadhi ya wamiliki wa mashamba na wachimbaji wadogo ambao ni wananchi walioko eneo la mgodi la Bulumbaka wamesema:
“Baadhi ya wenye mashamba hawajui leseni hii ilivyopatikana maana hawakushirikishwa, sisi wananchi ambao pia ni wachimbaji wadogo tunaomba haki itendeke, hatutaki mtu yeyote anyanyaswe,” alisema Bw.Masuke Sahani mkazi wa Bulumbaka
“ Sisi tuna kilio kikubwa na mgodi wetu tumeshangaa kwamba Mwananyanzala amepata leseni wakati sisi tuna muda mrefu tunatafuta hiyo leseni kwa watu wa madini hatujapata, tunaomba Mkuu wa Wilaya atusaidie sisi wakazi wa Bulumbaka tupate haki yetu,” alisema Monica Daniel mmoja wa wamiliki wa mashamba Bulumbaka.
Awali akizungumzia na wananchi hao walipofika ofisini kwake, Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga amesema malalamiko ya wananchi hao ameyapokea, ambapo amebainisha kuwa maagizo aliyayatoa awali hayakufuatwa hivyo akawaomba wauone uongozi wa mkoa ambao nao baadaye ukaelekeza ofisi yake iyashaghulikie kwa kuwa yako ndani ya uwezo wake.
Mmiliki wa leseni katika eneo la Bulumbaka Seni Mwananyanzala amesema kuwa leseni yake ilitolewa kihalali ambapo alifafanua kuwa leseni hiyo ilisainiwa tarehe 19 Machi 2021.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2021/04/malalamiko-ya-wachimbaji-wenye-mashamba.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa