Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Meatu Dkt.Joseph Chilongani pamoja na wataalam wa Halmashauri ya Meatu kutunga sheria ndogo zitakazosaidia kulinda na kutunza bwawa la maji la Mwanjoro.
Mhe. Makamu wa Rais amesema hayo leo wakati akizungumza na wananchi wa kata ya Mwanjoro mara baada ya kuweka jiwe la msingi katika Mradi wa bwawa la maji la Mwanjoro lililopo kata ya Mwanjoro Wilayani humo.
Mhe.Makamu wa Rais amesema Serikali inatambua uwepo wa tatizo la maji na ukame uliopo Wilayani humo ndiyo maana imeamua kujenga bwawa hilo litakalogharimu shilingi bilioni1.3 kwa awamu ya kwanza, hivyo ni lazima kuwepo na sheria ndogo zitasaidia kufanya bwawa hilo lidumu na kutoa huduma endelevu kwa wananchi
“Hili bwawa halitaki mifugo isogezwe huku wala shughuli za binadamu zije huku, nimemtaka Mkuu wa Wilaya na wataalam waweke sheria ndogo za kulinda bwawa na eneo linalozunguka bwawa, sheria zitakapo tungwa mzifuate, mkiliharibu mtakosa maji na mtarudi kule kule mlikotoka” alisisitiza Makamu wa Rais.
Ameongeza kuwa pamoja na Serikali kujenga Bwawa hilo kwa ajili ya matumizi ya binadamu na mifugo, kutokana na hali ya ukame ya wilaya hiyo Serikali imejipanga kujenga bwawa lingine litakalotumika kwa ajili ya shughuli za Kilimo cha Umwagiliaji.
Akitoa maelezo juu ya mradi huo, Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isack Kamwelwe amesema Sera ya Serikali ni kuwapunguzia wananchi adha ya kufuata maji umbali mrefu, hivyo kupitia mradi wa Mwanjoro wananchi wa Vijiji vya Mwanjoro, Mbushi na Jinamo watasogezewa huduma za maji karibu ili wasiende zaidi ya mita 400.
Aidha, amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Fabian Manoza kuwasilisha orodha ya mahitaji ya visima vya maji katika wilaya hiyo, ili viwekwe katika bajeti ya mwaka 2018/2019 , lengo likiwa ni kuongeza kiwango cha utoaji wa huduma za maji kwa wananchi wilayani humo.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Mbunge wa jimbo la Meatu Salum Khamis ameishukuru serikali kwa jitihada zote zinazofanyika katika kuondoa tatizo la maji na akaahidi kushirikiana na Wabunge pamoja na Wizara ya Maji kuhakikisha wananchi wa Meatu wanapata maji safi na salama.
Naye Mbunge wa Jimbo la Kisesa ambaye pia ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe.Luhaga Mpina akizungumza kwa niaba ya wananchi katika Mkutano wa Hadhara uliofanyika katika Kata ya Mwandoya ameomba Wizara ya Maji isaidie upatikanaji wa maji katika kata zote za Jimbo la Kisesa.
Makamu wa Rais anaendelea na ziara yake ya siku nne Mkoani Simiyu ambapo leo akiwa wilayani Meatu ameweka Jiwe la msingi mradi wa Maji wa Bwawa la Mwanjoro, amesalimia wananchi wa Kata ya mwanjoro, Mwanhuzi na kufanya mkutano wa hadhara katika Kata ya Mwandoya.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI KUHUSU HABARI HII FUNGUA HAPA:-https://simiyuregion.blogspot.com/2018/02/makamu-wa-raissheria-ndogo-zitungwe.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa