Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan amewapongeza viongozi wa Mkoa wa Simiyu kwa kuunga mkono jitihada za Serikali hususani katika utekelezaji wa Sera ya Tanzania ya Viwanda.
Mhe.Makamu wa Rais ametoa pongezi hizo wakati akizungumza na Wananchi wa Mji wa Bariadi kwenye Mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa CCM Mkoa wa Simiyu.
Amesema amepokea taarifa kuwa Mkoa wa Simiyu una jumla ya viwanda 14 vya kuchakata pamba na viwanda vidogo vya kuongeza thamani ya mazao 1035, jambo ambalo ni maendeleo makubwa kwa wananchi na akatoa wito kwa wananchi wa Simiyu kuendelea kuwekeza katika maeneo mbalimbali na kuwataka kuwapokea wawekezaji kutoka maeneo mengine ndani na nje ya nchi.
Aidha, amepongeza utekelezaji wa mkakati wa “Wilaya Moja Bidhaa Moja” ambao amesema ni mkakati mzuri unaoupambambanua Mkoa wa Simiyu katika Sekta ya Viwanda.
“Nimeelezwa hapa na Mkuu wa Mkoa kuwa mmeanza kwa kila wilaya moja kuwa na bidhaa moja(kiwanda kimoja) lakini haikatazwi wilaya hiyo kuwa na viwanda vidogo, nimeelezwa kuwa Meatu mmeamua kusindika maziwa na Maswa kiwanda cha chaki, Bariadi kiwanda cha bidhaa za afya zitokanazo na pamba na hiki ni kiwanda changu ninacho kisimamia” alisema
“Nataka kuahidi kuwa kiwanda hiki kitajengwa na kitazalisha bidhaa za sekta ya Afya, Busega pia kitajengwa kiwanda cha maji tunayotundikiwa hospitali(IV Infussion/drip), Itilima nimeambiwa ni masuala ya asali na alizeti, lakini pia nimeambiwa kuna viwanda vya bidhaa za ngozi maeneo tofauti nawapongeza sana kwa mwamko mkubwa huu” alisisitiza Makamu wa Rais.
Wakati huo huo Mhe.Makamu wa Rais amewapongeza viongozi wa Mkoa na Halmashauri ya Mji Bariadi kwa kusimamia na kuhakikisha barabara za Mjini Bariadi zinajengwa kwa kiwango kinachoridhisha, hivyo amesisitiza usafi uimarishwe katika barabara hizo hususani barabara iliyopewa jina lake ili kupendezesha Mji.
Katika hatua nyingine Mhe.Makamu wa Rais amewahakikishia wananchi wa Mkoa wa Simiyu upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama ifikapo mwaka 2019/2020, kupitia Mradi mkubwa wa Maji kutoka Ziwa Victoria ambao unatekelezwa na Wizara iliyo chini ya Ofisi yake kwa kushrikiana na Wizara ya Maji.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka amesema tarehe 21/02/2017Mhe. Makamu wa Rais atakutana na timu ya wataalam wanaofanya upembuzi yakinifu wa ujenzi wa Kiwanda cha bidhaa za afya zitokanazo na pamba mkoani humo, ambapo alibainisha kuwa mkoa umejipambanua kwenye sekta ya viwanda hasa katika kutekeleza maono na mtazamo wa Viongozi wakuu wa Kitaifa.
Mbunge wa Bariadi Andrew Chenge akawasilisha changamoto za wananchi kwa Makamu wa Rais amesema wananchi Bariadi wanakabiliwa na uvamizi wa tembo katika mashamba yao , hivyo ni vema ikawekwa mipaka na zikatafutwa njia ya kuwazuia, jambo ambalo Mhe. Makamu alilitolea ufafanuzi kuwa Serikali italifanyia kazi kuhakikisha wanyama hao hawawadhuru watu na kuharibu mazao.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe.Samia Suluhu Hassan akiwa katika ziara yake wilayani Bariadi ameweka Jiwe la Msingi Ujenzi wa Nyumba za Viongozi wa Mkoa wa Simiyu, amekagua ujenzi wa barabara za Bariadi Mjini na kufungua barabara moja iliyopewa jina lake”BARABARA YA SAMIA SULUHU”.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI KUHUSU HABARI HII FUNGUA HAPA:-https://simiyuregion.blogspot.com/2018/02/makamu-wa-rais-apongeza-viongozi-mkoani.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa