Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amekitaka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kuongeza ubora na kupanua wigo wa udahili wa wanafunzi kwenye programu za sasa ili kuendana na Sera Tanzania ya viwanda na kufikia Uchumi wa kati ifikapo 2025.
Ushauri huo ameutoa katika mahafali ya 34 ya Chuo Kikuu Huria cha TANZANIA yaliyofanyika katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu.
Makamu wa Rais amesema kuwa ili kuweza kufikia TANZANIA ya viwanda na kufikia uchumi wa kati 2025 lazima udahili wa wanafunzi katika vyuo vikuu ufikie kiwango cha angalau asilimia 23.
“Naungana na Mhe.Rais kuwaomba muisaidie nchi yetu kuongeza kiwango cha udahili wa wananchi wake kwa haraka na kwa kasi itakayotuwezesha kufikia lengo la kuwa nchi ya Uchumi wa kati ifikapo 2025” alisema
“Kwa mujibu wa takwimu za Benki ya Dunia kiwango kidogo cha udahili katika elimu ya juu ni sifa ya msingi ya Uchumi wa chini na wa kimaskini, Uchumi wa kati na wa Viwanda hauwezi kufikiwa na kuwa endelevu pasipokuwa na kiwango cha udahili katika elimu ya juu cha angalau asilimia 23” alisema Makamu wa Rais.
Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Mhe.William Ole Nasha amesema Serikali inatambua na kuthamini mchango wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania katika maendeleo ya sekta ya elimu nchini kwa kuwa kimekuwa mtekelezaji mkuu wa malengo na mikakati ya Serikali kwa upande wa ujifunzaji kwa njia za masafa.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Profesa Elifas Bisanda amesema tangu Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kianzishwe idadi ya wahitimu imefikia 38, 993 baada ya mahafali ya 34 idadi hiyo imeongezeka kufikia 39,934, jambo ambalo limechangia kukuza rasilimali watu hapa nchini.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu amesema kufanyika kwa mahafali ya 34 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania mkoani humo kutakuwa chachu na kutaleta mwamko mpya wa elimu kwa wananchi Mkoani humo.
“Tuliona tuwaalike wanafunzi ili kujenga hamasa kwao, tulialika kamati zetu za shule, madiwani, walimu na wananchi wote wa Simiyu ili washuhudie tukio hili tukiamini kuwa kwa kuona tukio hili kila mmoja atatamani kuwa hivyo kesho, kama siyo yeye basi awe mwanaye au ndugu yake” alisema Mtaka.
Jumla ya wahitimu 941 kutoka Tanzania bara na Zanzibar na nchi jirani walihudhurishwa mbele ya Mkuu wa Chuo Kikuu Huria Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda na kutunukiwa Astashaha, stashahada, shahada, shahada za uzamili , ambapo miongoni mwa hao 941 wahitimu saba walitunukiwa shahada ya uzamivu(PhD).
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI KUHUSU HABARI HII FUNGUA HAPA:-https://simiyuregion.blogspot.com/2018/02/makamu-wa-rais-akitaka-chuo-kikuu-huria.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa