Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt.Bashiru Ally amewataka wataalam wa ujenzi kuzingatia miundombinu ya uvunaji wa maji ya mvua katika usanifu wa majengo yote ya Chama na Serikali yanayoendela kujengwa hapa nchini, ili kupunguza gharama za uendeshaji zinazotumika kununua/kulipia maji na kuwa na uhakika wa upatikanaji wa huduma ya maji katika majengo hayo.
Ameyasema hayo Agosti 10, 2019 wakati akikagua maendeleao ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Bariadi na wakati akiweka jiwe la msingi ujenzi wa Ofisi ya CCM wilaya ya Busega mkoani Simiyu.
Amesema ikiwa majengo yote yatakuwa na miundombinu ya kuvuna maji ikiwa ni pamoja na kuwa na matenki imara ya kuhifadhia maji hayo, inapotokea maji yakakatika tunatumia maji yaliyovunwa lakini pia gharama za kuendesha ofisi hususani za kulipia huduma zinapungua.
“Naelekeza nchini nzima majengo yote mapya ya Chama kuanzia yale ya tawi, biashara na ofisi tuyasanifu kwa kuzingatia Miundombinu ya uvunaji wa maji ya mvua, na ndani ya Serikali nimemshauri waziri wa maji kuwa miongoni mwa mambo tunayotakiwa kuyafanya kukabiliana na changamoto ya maji ni ubunifu” alisema Dkt. Bashiru
Kuhusu zao la pamba amewataka viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuanzia ngazi ya tawi kuhakikisha wanafuatilia mwenendo wa ununuzi wa zao la pamba na kuwasilisha taarifa kwake lengo likiwa ni kuhakikisha wakulima wanapata haki yao.
“Sasa hivi Chama lazima kiwe mbele ya Serikali kutetea haki za wavuja jasho, nchi nzima machinery (watendaji wote ) ya chama lazima ifuatilie ununuzi wa mazao ya wakulima na mimi nipate taarifa za kila siku; maneno yamesemwa mengi tangu mwezi wa tano, mwezi wa sita na wa saba tumekaa vikao mwezi huu wa nane ni vitendo” alisema.
Kwa upade wake Mbunge wa Busega Mhe. Dkt. Raphael Chegeni amemshukuru Katibu Mkuu wa CCM Taifa Dkt. Bashiru Ally kwa kuielekeza Serikali kuimarisha usimamizi wa suala la ununuzi wa pamba, ambapo hadi sasa limeanza kupata ufumbuzi kwa wanunuzi kupewa fedha na benki kwa ajili ya kununua pamba kwa wakulima kwa bei elekezi ya shilingi 1200/=
Akitoa salamu za Serikali Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka ametoa wito kwa wananchi wa Wilaya ya Busega kutumia faida ya kuwa na Ziwa Victoria kufanya shughuli za uvuvi kwa kutumia vizimba na mabwawa na wakati huo huo amewataka kujihusisha na kilimo cha umwagiliaji ili kujihakishia usalama wa chakula.
Akiwa Wilayani Bariadi, Dkt. Bashiru alitembelea eneo la ujenzi wa Tawi la Chuo cha usimamizi wa Fedha(IFM) kijiji cha Sapiwi na kupongeza viongozi na wananchi wa Kijiji hicho kwa kuwa na matumizi bora ya ardhi ya kijiji chao jambo ambalo limepelekea kijiji kutoa eneo kwa ajili ya ujenzi wa chuo hicho ambacho kitawaletea manufaa wao kama jamii ya Sapiwi na Taifa kwa ujumla na kuwataka viongozi wengine kuiga mfano huo.
Dkt. Bashiru yuko katika ziara yake ya kikazi mkoani Simiyu kwa ajili ya masuala mbalimbali ya Chama na kufuatilia suala la mwenendo wa ununuzi wa pamba.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2019/08/dkt-bashiru-majengo-yote-mapya-ya-chama.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa