Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka amewaagiza Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri Mkoani humo kuunda timu zitakazopitia na kujiridhisha juu ya majina ya wanafunzi 633 waliotajwa kuwa Mamluki na kuondolewa shuleni kwa kukosa sifa za kusoma shule za sekondari za Serikali kutokana na sababu mbalimbali.
Agizo hilo amelitoa jana katika Shule ya Sekondari Nkoma wilayani ITILIMA kwenye kikao chake na viongozi, watendaji wa Serikali na wazazi wa baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo walioondolewa katika mfumo wa Serikali kutokana na kutumia majina yasiyo yao, kukosa fomu za TSM 9 , kukosa vibali vya kukariri/kurudia kidato na vibali vya uhamisho.
Mtaka amesema timu hizo zitakazoundwa kwa kila Wilaya zifuatilie na kujiridhisha kwa kupitia majina yote pamoja na sababu za wanafunzi hao kuitwa Mamluki na kuondolewa katika mfumo wa Serikali zilizoanishwa, ambapo amebainisha kuwa watendaji wa Idara ya Elimu watakaobainika kusababisha kwa uzembe wanafunzi hao kuondolewa shuleni watachukuliwa hatua za kinidhamu.
Ameongeza kuwa Wakuu wa Wilaya kwa kushirikiana na Wakurugenzi wa Halmashauri na Maafisa Elimu Sekondari waitishe vikao na wanafunzi hao na wazazi wao, ili wazungumze na kuwaeleza hatua zitakazochukuliwa baada ya kujiridhisha, baadaye taarifa ya kila wilaya iwasilishwe mkoani.
“Kufikia Ijumaa wakuu wote wa Wilaya na Maafisa Elimu wawe wamekutana na wanafunzi waliopata matatizo hayo,wazazi wao na watoto wote waitwe kutoa ushuhuda wa nini kimesababisha wao kuitwa mamluki na kurudishwa nyumbani, wakishajiridhisha watuletee hiyo taarifa na sisi Mkoa tutaipitia na kutoa maelekezo; tunaweza kusema wanafunzi 633 ni mamluki kumbe umamluki wa baadhi ya wanafunzi umesababishwa na uzembe wa Watendaji wetu.” alisisitiza Mtaka.
Aidha baada ya kusikiliza hoja za baadhi ya wanafunzi walioondolewa katika mfumo wa shule za Serikali pamoja na wazazi wao shuleni Nkoma na kubaini kuwa baadhi ya sababu zilizopelekea wanafunzi hao kuondolewa zimechangiwa na uzembe wa baadhi ya Watendaji wa Idara ya Elimu ngazi ya Wilaya na Wakuu wa Shule Mtaka ameagiza wanafunzi hao warudishwe shuleni mara moja.
“Kuna wanafunzi hapa Nkoma tumewasikiliza kesi zao wapo ambao walipaswa kurudia darasa , taratibu za upatikanaji wa kibali cha kurudia darasa kama wanafunzi pamoja na wazazi wamefanya, lakini inaonekana kuna uzembe kati ya Wakuu wa Shule na Idara ya Elimu Wilaya, maagizo ya Serikali ya Mkoa vibali vya wanafunzi hao kufikia tarehe 29/11/2017 viwe vimetolewa na warudishwe shuleni” amesema Mtaka.
Sanjari na hilo Mtaka ameagiza wanafunzi wote wanaosoma shule za Sekondari kwa kutumia majina ya watu wengine waondolewe katika mfumo wa shule za Sekondari za Serikali na akatoa wito kwa wazazi wao kuwapeleka katika shule binafsi au katika utaratibu wa utahiniwa binafsi (QT) ili wafanye mitihani kama watahiniwa binafsi (Private Candidates).
Baadhi ya wanafunzi waliondolewa katika mfumo wa Shule za Serikali katika Shule ya Sekondari Nkoma Wilayani Itilima kwa sababu mbalimbali ikiwemo ya kutumia majina ya watu wengine wamesema wako tayari kuendelea na masomo ikiwa watapata nafasi katika shule binafsi, ambapo wazazi wao pia wamesema wako tayari kuwapeleka watoto wao katika shule binafsi ili kuwasaidia wafikie malengo yao.
“ Nilipata taarifa kuwa mwanangu ameondolewa shuleni kwa sababu anatumia jina la mtu mwingine na nimeshaanza kutafuta nafasi kwenye shule za binafsi ili aendelee na masomo kwa sababu alikuwa anafanya vizuri darasani, kwa mfano muhula uliopita aliongoza” alisema Sumuni Daudi mmoja wa wazazi walioshiriki kikao na Mkuu wa Mkoa.
Naye Mbunge wa Jimbo la Itilima Njalu Silanga ameomba kuwepo na darasa maalum kwa wanafunzi watakaobainika kuwa siyo halali waandaliwe utaratibu wa kufundishwa na baadaye wafanye mitihani kama watahiniwa wa kujitegemea ili waweze kutimiza ndoto zao.
Wanafunzi waShule ya Sekondari Nkoma Wilayani Itilima pamoja na wazazi wao wakimsikiliza Mkuuwa Mkoa katika kikao maalum kilichofanyika shuleni hapo jana.
Wanafunzi waShule ya Sekondari Nkoma Wilayani Itilima pamoja na wazazi wao wakimsikilizaMkuuwa Mkoa katika kikao maalum kilichofanyika shuleni hapo jana.
Mbunge wa Jimbo la Itilima Mhe.Njalu Silanga akichangia hoja katika kikao kilichoitishwa naMkuu wa Mkoa wa Simiyu kwa lengo la kuzungumza na viongozi wa Serikali,wanafunzi walioondolewa shuleni kutokana na sababu mbalimbali pamoja na wazazi wao.
Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Mhe.Benson Kilangi akifuatilia kwa makini hoja mbalimbali zilizokuwa zikiwasilishwa katika kikao kilichoitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu kwa lengo la kuzungumza na viongozi wa Serikali , wanafunzi walioondolewa shuleni kutokana na sababu mbalimbali pamoja na wazazi wao wilayani humo.
Mmoja wawanafunzi walioondolewa shuleni kutokana na kukosa sifa za kusoma katika shuleza Sekondari za Serikali akizungumza mbele ya Mkuu wa Mkoa na viongozi wenginewa Serikali juu sababu ya kuondolewa shuleni.
Mmoja wa wazaziwa wanafunzi walioondolewa shuleni kutokana na kukosa sifa za kusoma katika shule za Sekondari za Serikali akizungumza mbele ya Mkuu wa Mkoa na viongozi wengine wa Serikali katika kikao kilichofanyika Shule ya Sekondari Nkoma wilayani Itilima kujadili suala hilo.
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa