Kukamilika kwa kiwanda cha ushonaji katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi kutasaidia kuongeza ajira, ujuzi na vipato vya wananchi wa Simiyu hususani wanawake na vijana.
Kiwanda hicho kinakadiriwa kujengwa kwa fedha kiasi cha shilingi milioni 85 hadi kukamilika kwake ambapo itatoa pia fursa kwa wakazi wa mji wa Bariadi na Mkoa mzima kwenda kujifunza ushonaji na ubunifu wa mitindo mbalimbali ya nguo ambayo baadae wataweza kujiajiri na kujiongezea kipato.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa kiwanda hicho mbele ya kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2018 Ndg. Charles Kabeho kabla ya kuweka jiwe la msingi kiwanda hicho ,Mhandisi wa Halmashauri ya Mji Samwel Msolini amesema Halmashauri ilipokea msaada wa vyerehani 50, kutoka Serikali ya Jamhuri ya China, vyerehani 25 vikiwa vya umeme na vingine 25 ni vya kawaida.
Ameongeza kuwa baada ya kupokea msaada huo Halmashauri imeamua kuanzisha Kiwanda hicho ili kuviwezesha kutumika na hatimaye Halmashauri ipate mapato, kutoa ajira kwa wananchi na wananchi kupata huduma za mavazi yenye kiwango.
“”Lengo la Ujenzi wa Kiwanda cha Ushonaji ni kwa ajili ya kushona nguo kwa mahitaji mbalimbali ikiwa ni pamoja na nguo zinazovaliwa kwenye sherehe mbalimbali, sare za shule na maeneo ya kazi, mradi huu ukikamilika utaongeza mapato ya Halmashauri, kutoa ajira kwa wananchi na wananchi watapata huduma ya mavazi” alisema Msolini..
Aidha, akiweka jiwe la msingi katika kiwanda hiki, kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2018, Ndg. Charles Kabeho amefurahishwa sana na akapongeza Halmashauri kwa kubuni mradi huo ambao amesema utakuwa na manufaa kwa wananchi na Halmashauri.
“Kiwanda hiki kitawasaidia wajasiriamali wanaojihusisha na masuala ya ushonaji kupata kipato, kitawasaidia wananchi kujiajiri wenyewe, lakini pia Halmashauri nayo itapata mapato” alisema Charles Kabeho..
Angello Michael mkazi wa mji wa Bariadi alisema kiwanda hicho kitasaidia vijana na wanawake wengi ambao hawana kazi za kufanya na kubadilisha maisha na vipato vyao kwa baadaye.
Katika hatua nyingine Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2018 amewapongeza Wananchi na Viongozi katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi kwa namna walivyoshirikiana katika ujenzi wa Miundombinu ya Elimu katika Shule ya msingi Kilulu na akatoa wito wananchi kwenda kujifunza ujenzi wa majengo mazuri yenye kiwango kwa gharama nafuu.
Aidha Mwenge wa Uhuru ukiwa katika Halmashauri Mji wa Bariadi, pamoja na kuweka Jiwe la Msingi la kiwanda cha ushonaji, umepitia miradi mingine katika Sekta ya Elimu, Afya, Mazingira, Sekta Binafsi na Ujenzi.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI KUHUSU HABARI HII FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2018/08/kiwanda-cha-ushonaji-kuajiri-vijana-na.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa