Wananchi mkoani Simiyu kwa mara ya kwanza wameshuhudia Tamasha la Pasaka na kuomba Mwandaaji wa Matamasha ya Nyimbo za Injili kuendeleza utaratibu huu wa kufanya matamasha wakati wa sikukuu mikoani.
Ombi hilo la wakazi wa Simiyu limetolewa wakati wa Tamasha la Pasaka mkoani humo lililofanyika leo katika Uwanja wa Halmashauri Mjini Bariadi na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi kutoka maeneo tofauti mkoani humo..
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi hao wamemshukuru Mwandaaji ya Tamasha hilo Mkurugenzi wa Msama Promotion Ndg.Alex Msama pamoja na viongozi wa Serikali Mkoani Simiyu kuona umuhimu wa kuandaa Tamasha hilo kwa kuwa nyimbo za injili zinazoimbwa na waimbaji mbalimbali wa Kitaifa na Kimataifa zinawafanya watu wasifu na kumwabudu Mungu na kuachana na mambo yasiyofaa.
“Tumelipokea kwa furaha sana tamasha hili na tunaomba leo isiwe mwisho kila mwaka liwepo; yaani kwetu ni kama zawadi maana tangu mkoa wetu uanze ni mara ya kwanza, hii ni dalili kuwa Mkoa wetu unatambulika na unapendwa,tunawashukuru viongozi wetu na tunamshukuru Msama kutuletea Tamasha la Pasaka” alisema Lilian Kagirwa mkazi wa Bariadi Mjini.
Naye, Daniford William mkazi wa Bariadi amesema wigo wa matamasha hayo utanuliwe na kuwawezesha wananchi katika mikoa yote nchini kupata ujumbe wa Neno la Mungu kupitia nyimbo za Injili katika nyakati tofauti kwa mwaka.
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe.Festo Kiswaga akitoa salamu za Mkoa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka amesema Msama Promotion afanye utaratibu wa kuandaa tamasha lingine kubwa mkoani Simiyu kwa kuwa wananchi hao wanampenda Mungu na wako tayari kumtukuza Mungu kupitia matamasha kama hayo.
“ Nichukue nafasi hii kuwakaribisha Msama Promotion na waimbaji wote wa nyimbo za injili mkoani Simiyu kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, huu ni mkoa mpya lakini ni mkoa wenye kasi kubwa ya maendeleo na niombe wakati mwingine mtuletee tamasha kama hili siku ya Sikukuu ya Krismasi au Pasaka ili watu wengi wapate nafasi ya kumtukuza Mungu zaidi ya ilivyokuwa leo ”.
Aidha ,Mkuu huyo wa Wilaya amesisitiza wananchi kuendelea kuliombea Taifa na viongozi wote ili kudumisha amani, upendo na mshikamano wa nchi.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Msama Promotion, Bwana Charles Mwakipesile amewashukuru na kuwapongeza wananchi wa Bariadi kwa mapokezi mazuri na akaahidi kuwa Kampuni hiyo itakuza vipaji vya baadhi ya waimbaji wa nyimbo za Injili walionekana kuwa na uwezo mzuri kufanya vizuri katika medani ya muziki wa injili.
Tamasha la Pasaka Mkoani Simiyu limehudhuriwa na Waimbaji wa Kitaifa na Kimataifa wakiwemo Upendo Nkone,Beatrice Mwaipaja,Upendo Kilahiro, Martha Mwaipaja, Jesca Honore, Sifael Mwabuka na kwaya mbalimbali kutoka katika Makanisa ya Mjini Bariadi.
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa