Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limewahakikishia viongozi wa Mkoa wa Simiyu kuwa litaanza kujenga majengo ya kudumu katika Uwanja wa Nanenane Nyakabindi Bariadi mkoani humo, mwishoni mwa mwaka 2018.
Haya yamesemwa na Mwakilishi wa Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Martin Busungu, Luteni Kanali Respicious Kaiza wakati Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Simiyu na viongozi wa Wilaya ya Bariadi wakiagana na baadhi ya viongozi na Maafisa wa JKT katika Uwanja wa Nanenane Nyakabindi mara baada ya kukamilisha siku tatu za nyongeza za maonesho ya nanenane zilizotolewa na Waziri wa Kilimo, Dkt. Charles Tizeba, wakati akifungua maonesho hayo Kitaifa mwaka 2018, mkoani Simiyu.
Luteni Kanali Kaiza amesema viongozi wa JKT wameondoka Nyakabindi Uwanja wa Nanenane kwa lengo la kwenda kujipanga ili waondokane na majengo ya kuhamisha na kuanza ujenzi wa majengo ya kudumu katika uwanjauwanja huo katika maonesho yajayo.
"Tutaka kwenda kujipanga baada ya muda kidogo tutarudi kuanza rasmi ujenzi wa majengo ya kudumu ili tusiwe na majengo haya ambayo ni ya kuhamisha, Mungu akijalia mwishoni mwa mwaka huu tunataka tuwe tumeshaanza kujenga"'alisema.
Aidha, Luteni Kanali Kaiza amesema pamoja na viongozi na Maafisa wa JKT kuondoka Uwanjani hapo, vijana wa JKT pamoja na viongozi wa JKT waliokuwepo katika Kambi ya Nyakabindi wakati wa Maonesho ya Nanenane watabaki katika Eneo hilo la Nyakabindi kuendeleza shughuli walizozianzisha katika Uwanja huo.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema dhamira ya Mkoa huo ni kuwa na Maonesho ya Nanenane ya Kimataifa hivyo amewaomba viongozi wa JKT kuona uwezekano wa kujenga majengo makubwa zaidi ya yaliyotumika mwaka huu kwa kuwa mwaka 2019 watu zaidi ya 100,000 wanatarajiwa kushiriki maonesho ya nanenane na akawaomba pia waone uwezekano wa kuanza kujenga majengo hayo mapema kuanzia mwezi Oktoba, 2018.
Mtaka ametoa wito kwa JKT pia kujenga hoteli, hosteli, kumbi za mikutano na miundombinu mingine muhimu katika eneo la Nykabindi kwa kuwa eneo hilo litatumika kwa maonesho ya nanenane, maonesho ya kilimo biashara kila baada ya miezi mitatu na Vyuo vingi vya Elimu ya Juu vitajengwa karibu na eneo hilo, hivyo majengo hayo yakijengwa yatasaidia na kurahisisha kutoa huduma katika eneo hilo.
Aidha, amesema Serikali imeandaa utaratibu wa kuliendeleza eneo la Uwanja wa Nyakabindi ambapo itatoa nafasi kwa vijana, watumishi wa Umma walio tayari kufanya shughuli zao katika kilimo na mifugo kwa usimamizi wa Wataalam wa Kilimo na mifugo ili liweze kutumika kwa manufaa.
Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini ameshauri kwa kuwa JKT liwekeze katika ujenzi wa hoteli na hosteli katika eneo la Nyakabindi kwa kuwa ina nguvu kazi ili watu wanapokuja kwenye maonesho wapate huduma ya malazi kwa urahisi ndani ya mkoa badala ya kutoka nje, lakini pia JKT waweze kufanya biashara kupitia uwekezaji huo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Bw. Melckizedeck Humbe amesema uwepo wa JKT utachangia mji huo kukua kwa kasi, huku akibanisha kuwa Halmashauri inatarajia kupima viwanja katika eneo la Nyakabindi lengo ni kufanya JKT na wawekezaji mbalimbali kujenga miundombinu yote muhimu karibu na Uwanja wa Nanenane ikiwemo vituo vya mafuta, hoteli, kumbi na hosteli.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI KUHUSU TUKIO HILI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2018/08/jkt-kujenga-majengo-ya-kudumu-uwanja-wa.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa