Naibu Katibu Mkuu wizara ya mambo ya ndani Ramadhani Kailima amesema kwa kutambua tatizo la uhaba wa nyumba za makazi ya askari nchini tayari serikali imetenga shilingi bilioni 10 kwa ajili ya kujenga nyumba 400 katika mikoa mbalimbali nchini ukiwemo mkoa wa Simiyu.
Naibu waziri Kailima ametoa kauli hiyo katika hafla ya uzinduzi wa nyumba 10 za makazi ya askari wilayani Maswa zilizokabidhiwa kwa jeshi la polisi na wakala wa barabara nchini -TANROAD baada ya kukamilika mradi wa ujenzi wa barabara ya Maswa – Shinyanga na kuongeza kuwa katika awamu ya kwanza zitajengwa nyumba 148 kwa gharama ya shilingi bilioni 3.7 na awamu ya pili nyumba 252 kwa gharama ya shilingi bilioni 6.3 ambapo mkoa wa Simiyu utapata nyumba 20.
Aidha Mhe Kailima amewataka watendaji wote ndani ya jeshi la polisi kuzingatia maadili na kuepuka vitendo vya rushwa ambavyo amesema vinaichafua serikali na kupandikiza chuki katika jamii.
“ Tukio hili linaashiria namna ambavyo serikali inawajali askari wake, ninazindua nyumba hizi 10 kwa ajili yenu, sasa ni matumaini yangu makazi haya mapya yatawapa ari ya kufanya kazi kwa bidii zaidi bila upendeleo wala uonevu wa aina yeyote”, alisema mhe Kailima
Pia naibu waziri kailima ameliagiza jeshi la polisi mkoa wa Simiyu kuhakikisha linaweka utaratibu mzuri wa kuzitunza nyumba hizo sambamba na kuandaa mpango wa kuyampima maeneo yote yanayomilikiwa na jeshi hilo.
Akitoa hotuba kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Simiyu, mkuu wa wilaya ya Bariadi Festo Kiswaga ameishukuru serikali kwa kutoa kipaumbele katika mgao wa nyumba hizo 10 kwa jeshi la polisi wilaya ya Maswa huku akiahidi kuendelea kusimamia nidhamu na uwajibikaji miongoni mwa watumishi umma mkoani Simiyu.
Naye Kamanda wa polisi mkoa wa Simiyu Deusdedit Nsimeki amewataka askari wote watakaopata nafasi ya kuishi kwenye nyumba hizo kuzingatia usafi na kuitunza vizuri miundombinu yake huku akiahidi kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kujiridhisha kama agizo lake linatekelezwa.
Jitihada za kuboresha makazi ya askari mkoani Simiyu zinatasaidi kudumisha hali ya amani na usalama halikadhalika kuongeza kasi ya kufikia malengo ya mkoa sambamba na ajenda ya taifa kufikia uchumi wa kati kupitia sekta ya viwanda.
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa