MKUU wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro, amewaonya baadhi ya watu wanaohamasishana kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii kuhusu kufanya maandamano bila kufuata utaratibu uliopo na kwamba kitendo hicho ni kinyume cha sheria.
IGP Sirro amesema hayo leo Februari 26 Mjini Bariadi Mkoani Simiyu mara baada ya kuzungumza na Viongozi na Askari wa Jeshi la Polisi pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Simiyu wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja mkoani humo.
Amesema kuna utaratibu wa maandamano unaoanisha maandamano halali na yasiyo halali akabainisha kuwa maandamano yasiyo halali yanaashiria uvunjifu wa amani na kutenda uhalifu, hivyo ikiwa maandamano yataashiria kutenda uhalifu kwa kuwa jeshi la polisi lipo kuzuia uhalifu na litahakikisha maandamano hayo hayafanyiki.
“Maandamano ambayo si halali njia yake ni kuyadhibiti na uwezo wa kudhiti tunao, wananchi wanataka maendeleo hawataki usumbufu na wale wanaotaka usumbufu watapambana na Jeshi la polisi; jambo la msingi nawaeleza wafuate utaratibu watoe taarifa sisi hatuna tatizo lakini wakitaka kufanya kwa vurugu wasije wakailaumu Serikali” alisema IGP Sirro.
“Naona kwenye mitandao wanasema lakini niwaambie tu kwamba kuvunja sheria ni rahisi lakini madhara yake huwa ni mabaya sana, nawaomba wazazi waendelee kuwapa malezi bora na wawasaidie watoto wao wasijiingize katika matukio ya kuvunja sheria” alisisitiza
Aidha, IGP Sirro amewataka askari wa Jeshi la Polisi kote nchini kuhakikisha wanafanya kazi zao kwa kufuata misingi ya sheria na taratibu za nchi ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanatenda haki kwa wananchi wanaowahudumia.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema Jeshi la Polisi Mkoani humo limechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza matukio ya uhalifu yaliyokuwepo katika miaka kadhaa iliyopita ambayo ni pamoja na mauaji ya watu wenye Ualbino, Vikongwe na ukataji wa mapanga.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI JUU YA HABARI HII FUNGUA HAPA:-https://simiyuregion.blogspot.com/2018/02/igp-sirro-awaonya-wanaotaka-kuandamana.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa