Rai imetolewa kwa Wakurugenzi wa Halmashauri zote mkoani Simiyu kuhakikisha kuwa wanakamilisha zoezi la utoaji wa vitambulisho vya matibabu kwa wazee kufikia mwezi Juni 2021, ili wazee waweze kupata huduma za matibabu katika vituo mbalimbali vya kutolea huduma za afya kama Serikali ilivyodhamiria.
Rai hiyo imetolewa Novemba 5, 2020 Mjini Bariadi na Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka katika uzinduzi wa Baraza la Ushauri la Wazee Mkoa wa Simiyu..
“Mkoa kupitia Halmashauri umefanya utambuzi wa jumla ya wazee 68,175 kwa lengo la kuhakikisha kuwa wanapatiwa huduma muhimu, hadi sasa jumla ya mabaraza 770 ya wazee yameundwa katika ngazi zote ; kuhusu upatikanaji wa vitambulisho vya matibabu bure, jumla ya wazee 18, 911 wamepatiwa vitambulisho hivyo ndani ya mkoa sawa na asilimia 28,’ alisema Kiswaga.
Mabaraza si ya kiitikadi hivyo kila mtu mwenye umri wa miaka sitini na kuendelea ana haki ya kujiunga na kuwa mjumbe wa Baraza la Wazee mahali alipo, huku akiahidi kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na Wazee na kukukutana na wazee mara kwa mara ili kuhakikisha kuwa inawasilikiza na mahitaji yao muhimu yanapatikana.
Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa, Bibi.Mwanahamisi Kawega amesema Ofisi ya Mkuu wa Mkoa itahakikisha inasimamia utekelezaji wa suala la ugawaji wa vitambulisho vya matibabu kwa wazee katika Halmashauri zote ili wazee wote waweze kuvipata kwa wakati.
Aidha Kawega ameongeza kuwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu itawaelekeza Wakurugenzi wa Halmashauri kuwaalika viongozi wa mabaraza ya wazee kualikwa katika mabaraza ya madiwani ili waweze kuwasilisha kero zao na kupatiwa ufumbuzi.
aye Meneja Mradi kutoka Shirika la NABROHO SOCIETY FOR THE AGED linalojihusisha na utetezi wa haki za wazee , Bw. Kubini Nkondo ameipongeza Serikali kwa namna inavyotoa kipaumbele kwa wazee na namna ilivyokomesha mauaji ya wazee.
"Wazee wamepitia changamoto nyingi ukizungumzia hata suala la mauaji ya wazee, takwimu awali zilikuwa juu sana lakini katika utawala huu tunazungumzia mauaji hayo kupungua mpaka kufikia 'digit' (tarakimu) moja, Mkoa wa Simiyu ambao ulikuwa ukitajwa katika Mkoa 10 inayoongoza kwa mauaji ya wazee sasa hivi haitajwi hata tena katika mikoa inayoongoza kwa mauaji hayo," alisema Nkondo.
Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la Mkoa wa Simiyu, Bw. Lameck Sendo amesema Baraza hilo litaendelea kushirikiana na Serikali katika kushughulikia haki mbalimbali za wazee huku akiomba Serikali kuitungia sheria Sera ya wazee ya mwaka 2003 ili iweze kutumika katika kuwaongoza pamoja na miongozo iliyopo.
Afisa Ustawi wa Jamii Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Bw. Daniel Mapunda amesema Mkoa wa Simiyu una takribani wazee 68,175, hivyo kwa mujibu wa Sera ya Wazee ya mwaka 2003 Baraza la Wazee la Mkoa litakuwa ni chombo maalum cha kuwasemea wazee na kushiriki katika maeneo mbalimbali ya kimaamuzi.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2020/12/halmashauri-zatakiwa-kukamilisha-utoaji.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa