Wanafunzi wa darasa la saba katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu wamemuahidi Mkuu wa mkoa Anthony Mtaka hawatamuangusha katika mtihani wa Taifa Septemba 11-12, kwa kuwa wamejiandaa vizuri na wanaimani watafanya vizuri.
Wanafunzi hao wa shule ya msingi Somanda A na B wametoa ahadi hiyo kwa niaba ya wanafunzi wote wa darasa la saba wa mkoa wa Simiyu, mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthoy Mtaka wakati akizungumza nao na kuwatakia heri katika Mtihani huo.
Wamesema wana imani ya kufanya vizuri kwa sababu hata Mtihani wa Mkoa Utilimilifu(Mock) walifanya vizuri, wameandaliwa vizuri kwa kupewa mazoezi na mitihani ya mara kwa mara na wamepata mbinu na maarifa mapya ya kujibu maswali ya mitihani kupitia kambi za kitaaluma zilizofanyika katika kila shule.
“Sisi tumejiandaa vizuri sana na nina uhakika tutafanya vizuri katika Mtihani wa Taifa kama tulivyofanya vizuri kwenye Mock, walimu wametuandaa vizuri tulikuwa na kambi ya kitaaluma ambayo imetusaidia kukutana na walimu tofauti waliotufundisha vizuri zaidi, tunamuahidi Mkuu wa Mkoa kuwa hatutamuangusha” alisema Luhinda Nalisha kutoka S/M Somanda A.
“Tumejiandaa vizuri na tumejipanga kufanya vizuri, pia tunamshukuru Mkuu wa Mkoa kuja kututembelea na kutupa mawaidha tutayafanyia kazi, shule ipo vizuri kitaaluma na nidhamu hivyo tuna uhakika wa kufaulu mtihani wa Taifa” alisema Bugumba Nindwa mwanafunzi wa Shule ya Msingi Somanda B
Akizungumza na wanafunzi hao, Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amewatakia mtihani mwema na kuwataka watumie mbinu walizopewa na walimu kufanya vizuri, huku akiwaonya kutojihusisha na vitendo vya udanganyifu wa aina yoyote.
Katika hatua nyingine Mtaka ametoa wito kwa wahitimu wa vyuo vikuu kufundisha masomo ya maandalizi ya Kidato cha kwanza(Pre-form one) kwa wanafunzi watakaohitimu darasa la saba kwa ajili ya kuwaandaa wanafunzi na masomo ya elimu ya sekondari.
Naye Afisa elimu Msingi Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Mwl. Christopher Ligonda akishukuru kwa niaba ya walimu amesema wanafunzi wameandaliwa vizuri na wamefundishwa vizuri na wako tayari kwa ajili ya mtihani na matarajio yao ni kupata ufaulu mzuri kama walivyoahidi wenyewe.
Mkoa wa Simiyu una jumla ya wanafunzi 29,248 wa darasa la saba wanaotarajia kufanya mtihani wa Taifa Septemba 11-12, mwaka huu, ambao kati yao wavulana ni 13, 594 na wasichana 15.654.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2019/09/wanafunzi-wa-darasa-la-saba-simiyu.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa