Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka ametoa wito kwa Chama cha Walimu Tanzania(CWT) kuja na majawabu ya kuwasaidia walimu kuacha kukopa katika taasisi za fedha zisizo rasmi ambazo hazijasajiliwa na wafanyabiashara binafsi ambao wamekuwa wakichukua kadi zao za benki (ATM) na kukaa nazo na kuwatoza riba kubwa.
Mtaka ameyasema hayo katika Mkutano wa ujirani mwema wa Viongozi wa Chama cha Walimu Tanzania(CWT) ulioshirikisha viongozi kutoka mikoa ya Simiyu, Kigoma,Shinyanga, Mwanza, Geita, Mara, Tabora na Kagera, Mkutano uliofanyika Oktoba 30, 2019 Mjini Bariadi.
Amesema ni vema walimu wabadilike na kutumia taasisi rasmi za fedha kuchukua mikopo badala ya kukopa kwa wafanyabiashara binafsi au taasisi za fedha zisizo rasmi(ambazo hazijasajiliwa) ili waondokane na mikopo inayowaumiza kwa kuwa na riba kubwa.
“ Kuna wafanyabiashara wanakaa na kadi za ATM za walimu wetu, wakati mshahara unapotoka wanaenda kuchukua fedha na wanabaki na hizo kadi, ni lazima CWT mje na majawabu ya kuwasaidia walimu wanaokopa nje ya mfumo wa kibenki usio rasmi kwa sababu CWT sasa hivi ina benki; vilevile Benki kuu, benki zote za biashara na HAZINA wana utaratibu wa mikopo kupitia mishahara yetu,” alisema Mtaka.
Aidha, Mtaka ameahidi kuwa katika Mkoa wa Simiyu, Viongozi wote watahakikisha wanawapa kipaumbele na hawatakuwa tayari kuona watumishi wa kada nyingine wakiwadhalilisha walimu
Naye Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Wenyeulemavu, Mhe.Stella Ikupa amewapongeza Chama cha Walimu kwa kuwajumuisha watu wenye ulemavu katika ngazi za uongozi na kusisitiza walimu kupata mafunzo ya elimu maalum ili waweze kuwasaidia wanafunzi wenye mahitaji maalum waliopo katika shule zao.
“Niwapongeze CWT kujumuisha walemavu katika uongozi pia iwapongeze walimu wote kwa kazi kubwa mnayofanya, mna mchango mkubwa kwa ustawi wa mtu mmoja mmoja, kada mbalimbali na jamii kwa ujumla, Serikali imeendelea kufanyia kazi changamoto mbalimbali za walimu, ikiwemo kuwapandisha madaraja ambapo hivi karibuni walimu 124,000 walipandishwa madaraja,” alisema Ikupa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Habari - MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbas amesema Serikali imehakikisha wananchi wanapata taarifa kwa wakati, hivyo imetungwa Sheria ya Haki ya Kupata Taarifa mwaka 2016, ili kuruhusu kila mwananchi kufahamu mambo mbalimbali yanayoendelea kuhusu utendaji wa Serikali.
Ameongeza kuwa Serikali imedhamiria kufanya mageuzi makubwa kiuchumi, ndio maana kuna utekelezaji wa miradi mikubwa kama mradi wa kufua umeme wa Julius Nyerere, na mradi wa reli ya kisasa, huku akibainisha kuwa pia Serikali inaendelea kununua ndege, kwa sababu ndege ni uchumi na zinasaidia kukuza sekta ya utalii nchini.
Naye Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania(CWT) Taifa, Mwl. Deus Seif amesema walimu wataendelea kuchapa kazi huku akiomba Serikali kuendelea kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwemo kutopandishwa madaraja na mishahara kwa wakati, malipo ya fedha za likizo, uhamisho na malimbikizo ya mishahara.
Akichangia hoja katika mkutano huo Kiongozi wa CWT kutoka wilayani Misungwi Mwanza, Mwl Rosemary Mboneko ameiomba Serikali iwasaidie walimu wanaoomba uhamisho kuwafuata wenza wao waruhusiwe ili kuepuka ndoa za masafa na kuwafanya watumishi hao wakafanya kazi kwa amani.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2019/11/cwt-tegueni-kitendawili-cha-walimu.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa