Shirika lisilo la kiserikali la Doctor with Africa CUAMM linalofanya kazi na Mkoa wa Simiyu kama mdau wa Afya katika masuala ya UKIMWI na Huduma za Afya ya Mama na mtoto limetoa msaada wa vifaa kinga (viambukuzi) kwa ajili ya kuunga mkono Serikali katika kukabiliana na maambukizi ya Virusi vya Corona.
Akikabidhi msaada huo Mei 06, 2020 mjini Bariadi kiongozi kutoka CUAMM Bi. Barbara Andreuzizi amesema Vifaa kinga hivyo vina thamani ya shilingi milioni nne ambapo amebainisha kuwa Shirika hilo pia limetoa msaada mafuta na gari litakalotumiwa na wataalam wa afya kutoa elimu ya tahadhari ya maambukizi ya Virusi vya Corona katika mkoa wa Simiyu.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini ameshukuru CUAMM kwa kutoa msaada huo ambao ni sehemu ya makubaliano ya wadau wa afya na serikali mkoani humo katika kukabiliana na Corona na kuiagiza Timu ya mkoa ya usimamizi wa huduma za afya kuhakikisha vifaa hivyo vinapelekwa haraka katika vituo vya kutolea huduma za afya kwa wakati.
“Tatizo la COVID 19 liliporipotiwa kama mkoa tulikutana na wadau tukakubaliana kujiandaa namna ya kukabiliana nalo katika maeneo ya utoaji elimu, vifaa kinga na vifaa tiba, tunawashukuru sana CUAMM kwa vifaa kinga hivi ambavyo naamini vitasaidia timu zetu za usimamizi wa Afya(CMT) za Wilaya na vituo vya kutolea huduma za afya,” alisema Sagini.
Aidha, Sagini amewataka wataalam wa afya ngazi ya Mkoa wakiongozwa na Mganga Mkuu wa Mkoa kusimamia mafuta na gari lililotolewa na CUAMM kwa ajili ya kutoa elimu kwa wananchi na kuhakikisha linafanya kazi iliyokusudiwa na elimu inawafikia wananchi inavyostahili mpaka maeneo ya vijijini.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dkt. Festo Dugange Simiyu inaendelea na jitihada mbalimbali kukabiliana na maambukizi ya virusi vya Corona ambapo amewashukuru CUAMM kutoa msaada wa vifaa kinga vitakavyosaidia katika utoaji wa huduma kwenye vituo vya kutolea huduma za afya na kutoa wito kwa wadau wengine kuendelea kuunga mkono na wananchi kuendelea kuchukua tahadhari.
Naye Mratibu wa Mpango wa kukabiliana na Maambukizi ya Virusi vya Corona Dkt. Khamis Kulemba amesema msaada wa vifaa kinga, mafuta na gari kwa ajili ya kutoa elimu ni muhimu sana kwa kipindi hiki, ambapo amebainisha kuwa wataalam wa afya watashirikiana na Shirika hilo kuhakikisha elimu ya tahadhari ya Corona inawafikia wananchi na vifaa kutumika ipasavyo.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI FUNGUA KINGANISHI HIKI KATIKA BLOG RASMI YA MKOA WA SIMIYU:-https://simiyuregion.blogspot.com/2020/05/cuamm-watoa-msaada-vifaa-kinga-simiyu.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa