Benki ya CRDB imekabidhi mfano wa hundi ya shilingi milioni 60 kama mchango wa udhamini wa Maonesho ya Nanenane Kitaifa mwaka 2020 yanayofanyika katika Viwanja vya Nyakabindi Bariadi Simiyu, Kanda ya Ziwa Mshariki inayoundwa na mikoa ya Simiyu, Mara na Shinyanga kuanzia 01 Agosti, 2020 mpaka 08 Agosti, 2020.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo Julai 30, 2020 Meneja wa Benki ya CRDB Kanda ya Ziwa, Bw. Lusingi Sitta amesema benki hiyo imekuwa mstari wa mbele katika kusaidia wakulima ambapo amesema benki hiyo imejipanga katika kuhakikisha kuwa wakulima wote wa pamba wanapata malipo yao kupitia akaunti za benki ya CRDB.
“Tumehakikisha kuwa AMCOS zote tumefungua nao akaunti kama CRDB tutahakikisha kwamba kila mkulima anayeuza pamba yake atalipwa kupitia akaunti yake ya CRDB na tumejipanga kwamba kila alipo mkulima wa pamba nasi tupo hapo ,” alisema Lusingi.
Aidha, Lusingi amesema CRDB imefungua tawi lingine katika Wilaya ya Meatu ambapo amebainisha kuwa benki hiyo imepeleka gari ambalo lina mahitaji yote muhimu katika utoaji wa huduma na wateja(wananchi ) hivyo wanaweza kupata huduma zote katika gari hilo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga kwa niaba ya Wakuu wa Mikoa ya Simiyu, Mara na Shinyanga ameishukuru benki ya CRDB kwa kukubali kuwa mdhamini Mkuu wa Maonesho ya Nanenane Kitaifa mwaka 2020 na kwa namna ambavyo imekuwa ikiwajali wateja hususani wakulima ambapo imetoa zaidi ya asilimia 60 ya mikopo kwa wanunuzi wa pamba msimu wa mwaka 2019/2020 ili pamba ya wakulima inunuliwe.
“Kuna maana kubwa sana kwa CRDB kudhamini maonesho ya nanenane kwa sababu, lengo la maonesho haya ni kuwasaidia wakulima wa kawaida kwenda kwenye ukulima wa kisasa, hivyo inapotokea CRDB inajitokeza kusaidia maonesho kufana, inaenda sambamba na lengo la nchi la kuinua wakulima wadogo wadogo kwenda kwenye ukulima wenye tija,” alisema Kiswaga.
Wakati huo huo Kiswaga amewahakikishia viongozi wa benki ya CRDB kuwa serikali itaendelea kufanya kazi na benki hiyo katika matawi yote huku akitoa wito kwa viongozi hao kutosita kuwaeleza viongozi wa serikali kila wanapohitaji msaada katika maeneo mbalimbali.
Katika hatua nyingine Kiswaga ametoa wito kwa wananchi kutoka mikoa ya Simiyu, Mara na Shinyanga inayounda Kanda ya Ziwa Mashariki ya Maonesho ya Nanenane pamoja na maeneo mengine ndani na nje ya nchi; kujitokeza kwa wingi kushiriki katika maonesho ya Nanenane Kitaifa huku akiwahakikishia kuwa maonesho hayo yatakuwa ya tofauti kuwataka watarajia kuona teknolojia mbalimbali zinazoleta mapinduzi katika kilimo.
Kauli Mbiu ya Maonesho ya Nanenane mwaka 2020 ni “KWA MAENDELEO YA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI CHAGUA VIONGOZI BORA 2020.”
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:https://simiyuregion.blogspot.com/2020/07/crdb-yakabidhi-hundi-ya-shilingi.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa