Bodi ya Ushauri ya Hospitali Teule ya Mkoa wa Simiyu imezinduliwa rasmi na kutakiwa kusimamia vema Hospitali hiyo ili kuhakikisha huduma za afya zinatolewa ipasavyo kwa wananchi.
Akizungumza katika uzinduzi huo ambao ulifanyika katika Ukumbi wa Hospitali hiyo Mjini Bariadi, mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini, Katibu Tawala Msaidizi anayesimamia Utawala na Rasilimaliwatu Chele Ndaki, amesema bodi hiyo inalo jukumu kubwa la kuisimiamia hospitali teule ya mkoa na kuhakikisha huduma za afya zinatolewa katika viwango vinavyotakiwa.
"Mnalo jukumu kubwa katika kuhakikisha kwamba huduma za afya zinazotolewa zinaendana viwango vya Serikali yetu, nafikiri hata ninyi mnaona namna viongozi wetu walivyolipa kipaumbele suala afya, lengo ni kuhakikisha wananchi ambao ndiyo waajiri wetu wapewe huduma nzuri na waendelee kufanya shughuli zao za uzalishaji" alisema Ndaki.
Amesema pamoja na kushauri juu ya namna hospitali inavyotoa huduma, bodi hiyo pia itakuwa na jukumu la kushauri uongozi wa hospitali na kutoa mapendekezo juu ya mambo mbalimbali yanayolenga kuboresha mazingira ya utendaji kazi kwa watumishi ili waweze kutoa huduma zinazotakiwa.
Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Hospitali Teule ya Mkoa wa Simiyu, Bw. Gigi Mathias amesema wajumbe wa bodi hiyo wamejiwekea mpango kazi utakaowazesha kutoa ushauri ili kuboresha mambo mbalimbali katika hospitali hiyo.
"Kama bodi tutaishauri Menejimenti ya Hospitali iweze kuboresha huduma kwa wananchi na watumishi pia kwa sababu kama watumishi hawataboreshewa huduma zao muhimu utendaji wao utakuwa hafifu; tutasimamia rasilimali zote za hospitali, pia tuna jukumu kama bodi kusimamia kandarasi zote na kuhakikisha zinafanya kazi kwa viwango” alisema Gigi.
“Kwa kuwa bodi hii ina wajumbe wengi ambao ni watumishi wa Serikali na wengine ni wastaafu ambao ni wazoefu katika nyanja mbalimbali nina uhakika tutaishauri Menejimenti ya Hospitali Teule ya Mkoa wa Simiyu katika masuala yote kwa lengo la kuboresha utendaji na utoaji wa huduma bora" alisisitiza.
Naye Mjumbe wa bodi hiyo Bw. Said Zongo amesema wajumbe wa bodi hiyo watafanya kazi ya kuishauri Menejimenti ya Hospitali Teule ya Mkoa kwa mujibu wa sheria na taratibu.
MWISHO.
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa