Balozi wa Indonesia hapa nchini, Prof. Dkt. Ratlan Pardede amesema moja ya malengo makuu ya ziara yake mkoani Simiyu ni kwenda kuona mkoa huo unavyozalisha pamba na kuona namna ya kuongeza ushirikiano kati ya nchi yake na Tanzania(Simiyu) katika biashara ya zao la pamba.
Balozi Pardede amesema hayo wakati wa kikao maalum kati yake na viongozi wa Serikali na baadhi ya wafanyabiashara wa Mkoa huo Mjini Bariadi.
"Nimekuja kuona Simiyu kama mkoa unaoongoza kwa kilimo cha pamba Tanzania, nijue namna mnavyolima, mnavyoichakata, lengo hasa likiwa ni kuongeza kiwango cha pamba inayonunuliwa na nchi ya Indonesia kutoka Tanzania, kwa kuwa nchi yetu inahitaji pamba kwa ajili ya viwanda vya nguo "
Amesema Indonesia inahitaji zaidi ya asilimia 90 ya pamba kama malighafi katika viwanda vilivyopo nchini humo ambayo huagizwa nje ya nchi hiyo, hivyo kutokana na Mkoa wa Simiyu kuwa kiongozi katika uzalishaji wa pamba nchini mkoa huo unaweza kuuza pamba yake nchini Indonesia.
Ameongeza kuwa ili pamba ya Tanzania iweze kununuliwa nchini Indonesia inapaswa kuzalishwa katika ubora unaotakiwa na kuuzwa kwa bei isiyokuwa ya juu zaidi ikilinganishwa na pamba kutoka katika mataifa mengine yanayozalisha pamba.
Mhe. Balozi ameyataja maeneo mengine ambayo Indonesia itaongeza ushirikiano na Tanzania hususani mkoa wa Simiyu kuwa ni mifugo, miundombinu na umeme hasa unaozalishwa kwa kutumia maji(Hydroelectric Power).
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, amemuomba Balozi Pardede kuwakaribisha wawekezaji kutoka Indonesia kuja kuwekeza mkoani humo katika ujenzi wa viwanda vya nguo(textile industries), huku akiwahakikishia upatikanaji wa ardhi bila malipo yoyote.
Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Ndg. Jumanne Sagini amemuomba Balozi wa Indonesia hapa nchini na Serikali ya Indonesia kuona uwezekano wa kuanzisha mafunzo kwa watumishi wa Simiyu, kuwezesha wafanyabiashara wa Indonesia kushirikiana na wenzao wa Simiyu katika masuala mbalimbali ya kibiashara.
Aidha, Sagini ameomba ushirikiano kati ya Tanzania na Indonesia kuendelea kuimarishwa katika ngazi ya Taifa na kwa Mkoa ambapo ameomba Balozi huyo kuona namna ya kusaidia Mkoa wa Simiyu kuwa na Mkoa au Mji pacha nchini Indonesia.
Mhe. Balozi Prof. Dkt. Ratlan Pardede yuko katika ziara ya kikazi mkoani Simiyu ambayo inatarajiwa kuhitimishwa Mei 17 mwaka huu
MWISHO
KUPATA HABARI ZAIDI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI HAPA:-.https://simiyuregion.blogspot.com/2018/05/balozi-wa-indonesia-aihakikishia-simiyu.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa