Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema mkoa huo umejiwekea malengo ya kuhakikisha zaidi ya asilimia 80 ya wananchi wake kuwa na kadi za bima ya afya ili kujihakikishia upatikanaji wa huduma za matibabu katika vituo vya kutolea huduma za afya hapa nchini.
Mtaka ameyasema hayo wakati ufunguzi wa Jukwaa la Ushirika Afya wa Mkoa wa Simiyu lililofanyika kwa lengo la kujadili namna wanachama wa Vyama vya Ushirika vya Msingi (AMCOS)wanavyoweza kujiunga na Bima ya afya na kupewa kadi kupitia vyama vyao na kama familia, ambalo limefanyika Machi 14, mjini Bariadi.
Amesema yeye kama Mkuu wa Mkoa atafanya vikao na wanachama wa AMCOS na makundi mbalimbali ya wananchi katika wilaya zote mkoani hapa na kuzungumza nao kuwaelimisha juu ya umuhimu wa kila mwananchi kuwa na Bima ya Afya kwa ajili ya matibabu.
Aidha, amesema atawaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kuwa katika Vyama vya Ushirika Vya Msingi ambavyo vinawapa nafasi ya kupata matibabu makubwa katika vituo vya kutolea huduma za afya vya binafsi na vya umma kwa gharama nafuu ya shilingi 76,800/= kwa mtu mmoja(mwanachama wa ushirika).
“Nitafanya vikao na wanachama wa AMCOS zote, wakulima, wafugaji, wajasiriamali, makundi yote ya wananchi kwenye mkoa wetu wa Simiyu, tuweze kuwaelimisha faida ya mwananchi wa mkoa wa Simiyu kuwa na bima ya afya, kubwa zaidi umuhimu wa kuwa kwenye ushirika ambao utamwezesha kupata matibabu makubwa kwa bei nafuu” alisema
Katika hatua Nyingine Mtaka amesema katika kipindi cha msimu wa pamba katika kila kituo cha kununulia pamba NHIF itaweka Afisa wake kwa ajili ya kusajili wakulima na wanachama wa vyama vya ushirika walio tayari, hivyo akatoa wito kwa viongozi walioshiriki jukwaa la ushirika afya kutoa taarifa na elimu kwa wenzao juu ya umuhimu wa suala hilo.
Mtaka pia ametoa wito kwa wakulima wote wa pamba kulipa kipaumbele suala la afya kwa kuchukua hatua ya kuwa na bima za afya ili waweze kuona manufaa ya Serikali kuboresha huduma za afya ikiwa ni pamoja na kujenga Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Hospitali za wilaya kwa kila wilaya na Vituo vingine vya kutolea huduma za afya.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Bernad Konga amesema NHIF ni wadau wakubwa mkoani Simiyu, hivyo wako tayari kutoa huduma bora na wanawafikia wananchi wa makundi yote mkoani hapa na watahakikisha wanatoa kadi za bima ya afya kwa wakati kwa wanachama wote watakaojiunga.
Katika jukwaa hili washiriki wamepata nafasi ya kuchangia michango mbalimbali huku wanachama wa AMCOS wakiunga mkono mpango huo wa kupata bima ya afya kwa gharama ya shilingi 76,800/= ili waweze kumudu gharama za matibabu.
“Mpango huu nimeupokea vizuri ila ninashauri elimu iendelee kutolewa zaidi na zaidi ili wanachama wote wajue umuhimu wa kuwa na kadi za bima ya afya na namna zitakavyowasaidia” Lucas Ephraim mshiriki kutoka AMCOS ya Dutwa Bariadi.
“ Binafsi niko tayari kujiunga na mfuko wa bima ya afya ili nipate hiyo kadi itakayonifanya niweze kutibiwa popote hapa Tanzania, lakini naomba tutakapolipia hiyo 76,800/= kadi zetu tuzipate mapema” Mmoja wa Wanachama wa Vyama vya Ushirika vya msingi, Bw. Magwashi Gandila
Mkoa wa Simiyu una vyama vya Ushirika Vya Msingi(AMCOS) zaidi ya 300 na Jukwaa hili limeazimia wanachama wa AMCOS wakawe mabalozi wazuri kuwahamasisha wananchi kujiunga na Bima ya Afya.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2019/03/asilimia-80-ya-wananchi-simiyu-kutumia.html
Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka(katikati) aizungumza na Meneja wa Wanachama kutoka NHIF(kushoto) na Mkurugenzi mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya(NHIF), Benard Konga, mara baada ya kumalizika kwa Jukwaa la Ushirika Afya Mkoa wa Simiyu lililofanyika kwa lengo la kujadili namna wanachama wa Vyama vya Ushirika vya Msingi (AMCOS) wanavyoweza kujiunga na Bima ya afya na kupewa kadi kupitia vyama vyao na kama familia, ambalo limefanyika Machi 14, mjini Bariadi.
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa