Wadau wa Nishati na Maji mkoani Simiyu wameiomba Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kuangalia namna ya kuwasaidia wananchi wanaotumia chupa za maji kusafirisha mafuta vijijini na badala yake watafute njia mbadala ili kuepusha majanga ya moto na uchakachuaji wa nishati hiyo.
Wadau hao wametoa ushauri huo katika mkutano baina ya watendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) uliolenga kuelimisha wadau Mkoani Simiyu kuhusu majukumu ya Mamlaka hiyo, uliofanyika Mjini Bariadi Februari 21, 2019.
Wakizungumza katika mkutano huo wamesema kutokuwepo vyombo maalum vya ubebaji wa mafuta ya taa , petroli na diseli ni Moja ya tatizo kubwa, hivyo ni vema (EWURA) ikaja na njia mbadala ya kuwawezesha wananchi kusafirisha kwa usalama nishati hiyo.
“Tunaomba EWURA isaidie kuja na namna bora, vifaa vidogo vitakavyouzwa kwa bei rahisi ili wananchi waweze kusafirisha na kuhifadhi kwa urahisi kwa sababu yanawasaidia sana” amesema Mkaguzi wa Jeshi la Zimamoto Wilaya ya Bariadi, Maulo Kigahe.
Katika hatua nyingine wadau hao wamezungumzia suala la urasimu katika kuunganishwa kwa umeme kwa wananchi katika baadhi ya ofisi za Mameneja wa TANESCO na kuomba EWURA ione namna ya kuwasaidia wananchi wasaidiwe kupata huduma kwa wakati.
“ Kuna wananchi wakitaka kuunganishiwa umeme majumbani kwao wanadaiwa pesa mara shilingi laki tano, mara milioni moja hivi EWURA wanayajua matatizo haya? Tukizingatia kuwa umeme ni moja ya huduma muhimu kwa mwananchi tubadilike maana hata kule vijijini tulikozaliwa tunahitaji umeme” alisema Mkuu wa Gereza Wilaya ya Bariadi, Kajungu Massami.
Naye Saibogi Mwandu mwananchi kutoka Bariadi amesema ni vema wafanyabiashara wadogo hususani wanaouza mafuta ya petroli kwenye chupa wakapewa elimu ya namna ya kutunza mafuta hayo kwani wengi wao wamekuwa wakitunza bidhaa hiyo ndani.
Kwa upande wake Afisa Mkuu wa Mawasiliano (EWURA) makao makuu Wilfred Mwakalosi amesema EWURA katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita imeshabuni mwongozo utakaosaidia wawekezaji wa vijijini kuwekeza kwenye vituo vya gharama nafuu.
Akifunga mkutano huo Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe Festo Kiswaga kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amewataka wadau wote kuwa mabalozi wazuri wa EWURA ili wasaidie kufikisha elimu waliyoipata katika maeneo yao.
Awali akifungua mkutano huo, Kiswaga amesema Mkoa wa Simiyu umejipanga katika utekelezaji wa Sera ya Viwanda kwa kujenga viwanda ikiwemo kiwanda cha vifaa tiba, kiwanda cha chaki na vingine ambavyo vitahitaji huduma za nishati na maji , hivyo ameiomba EWURA kushirikiana na Taasisi zinazohusika na utoaji wa huduma hizo katika kuhakikisha zinatolewa katika viwango vinavyokidhi mahitaji ili Mkoa uweze kufikia malengo yake katika uzalishaji katika viwanda.
MWISHO.
KUPATA PICHA ZAIDI KUHUSU HABARI HII FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2019/02/wadau-waiomba-ewura-kuwasaidia-wananchi.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa