Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amezindua kampeni ya Shirika la Simu Tanzania (TTCL) Rudi Nyumbani Kumenoga mkoani humo na kuipongeza TCCL kwa kuboresha huduma zake na kuwa miongoni mwa mashirika ya Serikali yanayotoa gawio kwa Serikali, fedha ambazo zinasaidia kuboresha huduma za jamii na miundombinu.
Akizindua kampeni hiyo jana jioni Septemba 21, 2018 Mjini Bariadi, amesema kwa mara ya kwanza TTCL imetoa gawio kwa serikali fedha ambazo sehemu zimewezesha ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ulioanza na Jengo la Wagonjwa wa nje (OPD), ujenzi wa Barabara, miundombinu mingine pamoja na huduma mbalimbali kwa jamii.
Aidha, Mtaka ametoa wito kwa wananchi kutumia huduma za TTCL na kumuomba Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL Bw. Waziri Kindamba kufungua ofisi mkoani Simiyu, kumleta meneja na kuongeza watumishi ili kuongeza wigo wa utoaji wa huduma.
Ameongeza kuwa Mtendaji Mkuu wa TTCL aimarishe mfumo wa intaneti zaidi ili kuwezesha mpango wa mkoa wa Simiyu wa kufundisha kupitia teknolojia ambapo mtandao wa intaneti utahitajika kwa kiasi kikubwa.
“Tungehitaji tuone wanafunzi wa Simiyu wasome saa 24, wanafunzi wasio na walimu wa kutosha wa sayansi tutajenga vyumba vya madarasa vitakavyowezesha wao kusoma kupitia mfumo wa teknolojia, Mtendaji Mkuu wa TTCL imarisha mtandao wa TTCL wanafunzi wapate intaneti ili tuweze kurahisisha ufundishaji kwenye miji mikuu ya wilaya zetu” alisema.
Wakitoa maoni yao huduma za TTCL baadhi ya wananchi wa Mkoa wa Simiyu wamesema walikuwa hawazitumii lakini baada ya shirika hilo kuboresha huduma zake hasa za mtandao wa intaneti wameanza kuzitumia na wakaomba ziendelee kuboreshwa zaidi.
“ Mimi nilikuwa sijawahi kutumia mtandao wa TTCL nilikuwa natumia mitandao mingine tu lakini nilivyoona matangazo nikasema ngoja nijaribu, nikaenda kununua laini na kuanza kutumia, napenda kutumia zaidi intaneti yao iko vizuri” alisema Emmanuel Elias mkazi wa Bariadi
Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL Bw. Waziri Kindamba ametoa wito kwa Watanzania wote kurudi nyumbani na kuendelea kutumia huduma za TTCL kwa kuwa kadri wanavyotumia huduma hizo wanazalisha faida ambayo itaendelea kutumika hapa nchini kwa maendeleo ya nwananchi na Taifa kwa ujumla.
Aidha, kutokana na Taarifa ya kuwa na siku nne za maombolezo kwa Taifa ililotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kufuatia ajali ya Kivuko cha MV Nyerere huko Ukerewe Mkoani Mwanza, Mkurugenzi Kindamba amesema TTCL haitaendelea na kampeni hiyo RUDI NYUMBANI KUMENOGA mpaka siku hizo zipite ili kuungana na Watanzania wengine kuomboleza juu ya msiba huu wa Taifa.
“Mhe. Rais ametangaza siku nne za maombolezo kuanzia Septemba 21 hadi Septemba 24, 2018 kufuatia ajali ya kuzama kwa Kivuko cha MV Nyerere, tulikuwa tumepanga kuanza na Simiyu, twende Kahama halafu Tabora lakini kwa sababu ya msiba huu uliotugusa Watanzania wote na kwa kuwa Shirika hili ni la Watanzania na sisi tumeguswa hivyo itabidi shughuli hii tuisitishe kwa muda; Mungu awarehemu wenzetu waliotangulia na majeruhi wapone haraka” alisema.
MWISHO
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa