Naibu waziri ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana na Ajira, Mhe. Anthony Mavunde ametoa wito kwa kwa Chama cha wanataaluma na wajasiliamali wa Kanisa la Wadventista Tanzania (ATAPE) kushiriki katika uchumi wa viwanda ili kuongeza nafasi za ajira kwa vijana na kupunguza umaskini.
Mavunde ameyasema hayo wakati akifungua mkutano wa 20 wa chama hicho ambao Kitaifa unafanyika mkoani Simiyu na kuhudhuriwa na zaidi ya wanachama 1500 kutoka maeneo yote nchini.
“ATAPE kupitia wataaluma na wajasiriamali mnayo nafasi kubwa ya kukusanya rasilimali na kuhakikisha mnafanya vitu vyenye mchango chanya kwa Taifa hususani katika kutengeneza ajira kwa vija na kupunguza umaskini”
“Angalieni fursa zinazowazunguka ili miaka 20 ya uwepo wa ATAPE iende sambamba na uwekezaji na mafanikio mtakayoyapata, nitoe wito msiwe nyuma kushiriki katika ujenzi wa uchumi wa viwanda, Simiyu wanajenga viwanda vikubwa Maswa cha chaki na vifungashio, watajenga kiwanda cha vifaa tiba amkeni changamkieni” alisema Mhe. Mavunde.
Hata hivyo ameongeza kuwa serikali inatambua mchango mkubwa walioutoa ATAPE kwa kuendelea kutengeneza nafasi za ajira kupitia uwekezaji walioufanya kwenye meaneo mbalimbali ikiwemo kilimo, misitu na utoaji wa elimu ya ujasiliamali bure hatua iliyopelekea idadi kubwa ya watanzania kujiajiri pasipo kusubiri kuajiriwa.
“ATAPE imethubutu nitoe wito kwa madhehebu mengine kuiga mfumo huu wa kuwaleta pamoja wanataaluma na wajasiriamali ili wawe chachu ya mabadiliko kiuchumi waweze kufanya vitu vyenye manufaa kwa waumini na jamii kwa ujumla, epukeni dhana potofu ya kusema hatutoweza mjiamini mtaweza tu”alisema Mavunde.
Awali akimkaribisha Naibu waziri, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka amesema kuwa kama mkoa uliona kila sababu ya kuzialika taasisi mbalimbali ikiwemo BRELA , Shirika la bima la Taifa , EFTA lengo likiwa kuwafikia wajasiliamali na kuongeza kuwa ni vema wana ATAPE wakajifunza kutenda badala ya kuzungumza
“Ifike mahali mtofautishe mahubiri na ujasiliamali ni lazima mkizungumza mjifunze kutenda ….hivi karibuni ujenzi wa chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) utaanza, wanachuo 1000 wanatarajiwa kusoma hapo, nendeni pale mkajenge hosteli punguzeni porojo” alisema Mtaka.
Aidha, Mtaka ametoa wito kwa Wajasiriamali kusajili biashara zao ili ziweze kutambuliwa na wazikatie bima kwa ajili ya kuepuka hasara pindi biashara zao zinapokumbwa na majanga hususani majanga ya moto.
Mwenyekiti wa ATAPE Taifa, Bw. Freddie Manento amesema kuwa chama hicho kimefanikiwa kuwekeza zaidi ya shilingi bilioni moja kupitia miradi ya maendeleo waliyowekeza katika maeneo mbalimbali hapa nchini na kuongeza kuwa wamewekeza kwenye miradi ya kilimo afya, maji, ujasiliamali na elimu.
“Tuna mashamba zaidi ya ekari 10,000 ambayo tumelima korosho ,miti na mihogo ,tumewekeza mradi wa maji kigamboni jijini Dar es salaam hivyo tunavyoadhimisha miaka hii 20 ya ATAPE tuna kila sababu ya kujivunia maana miradi hii yote imetoa ajira nyingi kwa watanzania wenzetu zikiwemo za kudumu na za mkataba” alisema Maneto.
Kwa upande wake Askofu wa Kanisa la Waadventista Wasabato, Mark Malekana amewataka waumini wa kanisa hilo kufanya kazi kwa bidii ili kukwepa dhambi ya umaskini na kuwataka kuunga mkono juhudi za Serikali iliyopo madarakani katika kujiletea maendeleo.
Naye Irene Kweka ni miongoni mwa wajasiriamali walioshiriki mkutano huo amesema kuwa mkutano huo umemsaidia kuongeza wateja wapya kujifunza kupitia kubadilishana uzoefu sambamba na kuongeza kipato.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2019/04/naibu-waziri-mavunde-atoa-wito-kwa.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa